BAADA ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya 'AFCON Women’s Futsal Cup of Nations 2025' kwa kuifunga Senegal mabao 3-1, katika mchezo uliopigwa juzi, Uwanja wa Sportif Prince Moulay Abdallah, nchini Morocco, Kocha Mkuu wa timu ya wanawake wa Futsal ya Tanzania, Curtis Reid, ametamba kuwa haiogopi timu yoyote atakayopangwa nayo kwenye hatua hiyo.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo jijini Rabat, amesema anajivunia kikosi chake kwa kubadilika na kimecheza kwa uwezo mkubwa dhidi ya Senegal, hivyo kinampa matumaini ya kufanya vyema zaidi.
"Wamecheza vizuri sana, yale makosa yaliyoonekana kwenye mchezo uliopita hayakuwapo, walicheza kwa nidhamu kubwa. Tumekwenda nusu fainali, sisi tumejiandaa kucheza na yoyote yule, kwa jinsi wachezaji wangu walivyocheza mechi hii kwa uwezo na nidhamu kubwa, siogopi timu yoyote ile, nadhani wasichana hawa wako tayari," alisema kocha huyo.
Mabao ya Tanzania yaliwekwa wavuni na Donisia Minja, Vaileth Nicolaus na Anna Katunzi, huku nyota wa mchezo akiwa golikipa wa timu hiyo, Naijat Idrisa.
Akizungumza baada ya kupewa tuzo yake, Naijat, alisema ameipata kutokana na ushirikiano na wachezaji wenzake, huku akiahidi kuwa watapambana wafike fainali.
"Najisikia faraja sana, haikuwa rahisi, lakini tumepambana, kwa hali hii nina imani tutafika fainali," alisema kipa huyo.
Tanzania imeongoza kwenye Kundi C, ikiwa na pointi nne, huku wenyeji Morocco na Cameroon wakifuzu kwenye Kundi A, Angola ikifuzu kutoka Kundi B.
Timu Misri kutoka Kundi B, Madagascar, iliyoshika nafasi ya pili, Kundi C, zitacheza mechi ya mchujo kupata timu ya nne itakayotinga hatua ya nusu fainali.
Kombe la Mataifa ya Afrika la Futsal kwa Wanawake 2025 ni toleo la kwanza la michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake barani Afrika, yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Mashindano hayo pia yatatumika kama mchujo wa Afrika kwa ajili ya Kombe la Dunia la Futsal kwa Wanawake la FIFA 2025 litakalofanyika Ufilipino.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED