Simba: Hili tunalibeba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:28 PM Apr 28 2025
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua (katikati), akiwatoka wachezaji wa Stellenbosch FC ya Afrika Kusini katika mchezo wa marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa Uwanja wa Moses Mabhida, Durban
Picha: Mtandao
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua (katikati), akiwatoka wachezaji wa Stellenbosch FC ya Afrika Kusini katika mchezo wa marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa Uwanja wa Moses Mabhida, Durban

BAADA ya kushuhudia Simba ikitinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, uongozi wa klabu hiyo umeweka wazi kuwa ubingwa msimu huu wanaubeba.

Simba jana iliandika historia ya kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo kwa kuibana mbavu Stellenbosch FC ya Afrika Kusini kwa kuilazimisha suluhu kwenye Uwanja wa Moses Mabhida mjini Durban.

Matokeo hayo yameifanya Simba kutinga hatua hiyo kwa idadi ya bao 1-0 baada ya kupata ushindi huo kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopata katika uwanja wa New Amaan.

Akizungumza baada ya mechi jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Zubeda Sukuru, alisema wamejizatiti msimu huu kubeba ubingwa huo.

"Kauli mbiu yetu sasa hivi ni 'Hili tunalibeba', nawapongeza sana wachezaji na benchi la ufundi kwa kazi kubwa waliyoifanya, tunaenda kujipanga sasa kwa fainali na msimu huu tunalichukua hili kombe," alisema Sakuru kutoka Durban, Afrika Kusini.

Jana, Simba imerudia ilichokifanya mwaka 1993, ilipotinga hatua hiyo, kwa kutoka suluhu dhidi ya Atletico Sport Aviacao katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la CAF, ambalo sasa linaitwa Kombe la Shirikisho, baada ya ushindi wa mabao 3-1 iliyoupata, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam (sasa Uhuru), kwa mabao mawili ya Edward Chumila na Malota Soma, wageni wakipata bao lao kupitia kwa Nelo Miguel.

Katika mchezo wa jana ambao ulikuwa mgumu na wenye upinzani mkubwa, Simba ilifanikiwa kuhimili presha ya wapinzani wao na kucheza kwa utulivu mkubwa.

Ni wazi matokeo ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali uliochezwa, Aprili 20, Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, Simba ikishinda bao 1-0, ndilo lililoivusha na kwenda fainali baada ya jana kutoka 0-0.

Haikuwa rahisi hata kidogo kwa wawakilishi hao wa Tanzania kutinga hatua hiyo, kwani ilikumbana na mechi ngumu zaidi kuliko iliyochezwa mjini Zanzibar.

Kipindi cha kwanza, Simba ilitawala mpira dakika 20 za kwanza, lakini baada ya hapo wapinzani wao waliouchukua mchezo na kufanya mashambulizi hadi mapumziko, wakipata kona kadhaa dakika za mwisho.

Alikuwa Kibu Denis, alipoanza kulitia msukosuko lango la Stellenbosch, aliingia na mpira ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake liliwababatiza mabeki wa timu hiyo na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Dakika ya nne, kipa wa Simba, Moussa Camara, alilazimika kufanya kazi ya ziada, alipokwenda juu ya vichwa vya wachezaji wa Stellenbosch na kupangua mpira mrefu wa kurushwa, ambapo katika purukushani hiyo aliumia, ingawa baadaye alinyanyuka na kuendelea na mchezo.

Stellenbosch, waliendelea kusukuma mashambulizi kwenye lango la Simba, ambapo dakika ya 20 na 22 nusura wapate mabao, lakini mabeki wa Simba wakiongozwa na Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue walikaa imara kuokoa hatari hizo.

Dakika ya 35, Mohamed Hussein 'Tshabalala' alifanya kazi ya ziada alipouwahi mpira uliokuwa unakwenda kwa Thato Khiba akiwa katika nafasi nzuri ya kumsababisha Camara aliuingilia mpira huo na kupiga kichwa cha kubembeleza kumrudishia kipa wake.

Camara aliiokoa tena Simba, alipopangua mpira uliopigwa kwa kichwa na Oliver Toure, dakika ya 40, kabla ya kufanya hivyo tena  dakika ya 45, akiuwahi mpira mrefu wa kurushwa usimfikie, straika hatari wa Stellenbosc, Andre De Jong.

Kipindi cha pili hasa dakika za mwisho, Kocha Fadlu Davids alifanya mabadiliko ya kiufundi, alimtoa Elie Mpanzu, ambaye alifanya shambulizi moja la hatari dakika ya 73, shuti kali kupanguliwa na kipa, Oscarine Masuluke na kuwa kona tasa, pamoja na Tshabalala, akawaingiza Valentin Nouma na beki aliyekuwa majeruhi kwa kipindi kirefu, Fondoh Che Malone ili kuimarisha ulinzi.

Mabadiliko hayo yalifanya kazi, kwani hadi kipenga cha mwisho kilichopulizwa na mwamuzi Mohamed Maarouf Eid Mansour mechi ilikuwa suluhu, ikiashiria Simba kutinga fainali.

Fainali za kombe hilo zitatarajiwa kupigwa, Mei 17, Simba ikiwa ugenini na marudiano ni Mei 25, ambapo mechi itachezwa  hapa nchini.

Katika fainali hiyo, Simba wana nafasi kubwa ya kukutana na RS Berkane ya Morocco ambayo jana ilikuwa ikicheza mchezo wake wa marudiano dhidi ya Costantine huku ikiwa mbele kwa mabao 4-0 waliyoyapata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wiki iliyopita.