Mwenyekiti wa CCM Kibiti atoa neno chama kushika dola
By
Julieth Mkireri
,
Nipashe
Published at 10:06 AM Apr 28 2025
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibiti, Juma Ndaruke.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibiti, Juma Ndaruke, amewataka wanachama wa chama hicho kuweka maslahi ya chama mbele kwa kusaidia juhudi za kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola.
Akizungumza mjini Kibaha wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Jimbo kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025, Ndaruke aliwahimiza wanachama kuepuka tabia ya kusemana vibaya, akieleza kuwa tabia hiyo inaweza kuleta vikwazo katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu.
Katika mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Sylvestry Koka, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa kipindi cha miaka mitano.
Ndaruke, aliyekuwa akimuwakilisha Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani, alisema:
"Tukitaka kusaidia chama chetu kiendelee kushika dola, tunapaswa kuwa wamoja na kuunga mkono viongozi wanaoleta maendeleo katika maeneo yetu. Haiwezekani Katibu wa Kata kazi yake iwe ni kumtukana Diwani. Hii si sawa. Baadaye jina likirudishwa kwa ajili ya kugombea tena, itakuwa vigumu kumpigia debe." Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, Sylvestry Koka.
Aidha, aliwasihi wanachama kusifu na kueleza mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa Ilani ya Chama badala ya kusemana vibaya, akisisitiza kuwa kufanya hivyo kunazidisha mshikamano na kuimarisha chama.
"Tupime tunapozungumzia viongozi wetu, tuchague sehemu sahihi za kusema mambo yetu. Ukimsema vibaya kiongozi, umeharibu taswira ya chama chetu na utaleta ugumu mkubwa wakati wa kampeni," aliongeza.
Katika hatua nyingine, Ndaruke alimpongeza Mbunge Koka kwa juhudi zake katika kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwatetea wananchi wake bungeni, hali iliyochochea maendeleo katika Jimbo la Kibiti.
Naye Mwenyekiti wa CCM Kibiti, Mwajuma Nyamka, alieleza kuwa miradi mingi ya maendeleo iliyotekelezwa katika eneo hilo ni matokeo ya juhudi za Mbunge Koka, ambaye amekuwa akishirikiana kwa karibu na viongozi wa ngazi zote, kuanzia mtaa hadi wilaya.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa kipindi cha 2020-2025, Mbunge Koka alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mahiri na usikivu mkubwa kwa kero za wananchi, pamoja na usimamizi wake wa miradi ya maendeleo.
Mbunge huyo aliwaomba wananchi kuhakikisha mwezi Oktoba wanampigia kura za heshima Rais Samia ili aendelee kuongoza Serikali kwa awamu nyingine.