MIKAKATI ya kumjenga mwanafunzi kimaisha kabla ya kumaliza elimu, kujumuisha kumfundisha ujasiriamali na stadi zinazofanana nazo mwanafunzi, asitumie badala ya kuwa tegemezi.
Ni mkakati unaowezesha wanafunzi wa ngazi ya elimu ya msingi na sekondari, kufanya ujasiriamali wanapokuwa nyumbani kusubiri matokeo ya mitihani, nyakati za likizo, au wakishamaliza masomo.
Kutekeleza taasisi isiyokuwa ya kiserikali, mwaka huu ikitimiza miaka 10 tangu kuanzishwa, inatekeleza mkakati huo kupitia mradi unaoitwa ‘Uwezo Award,’ ikijikita kuwapa nafasi wanafunzi wa sekondari kujifunza ujasiriamali kwa vitendo shuleni.
Mratibu wake, Noelle Mahuvi, anasema mradi huo unaendeshwa kwa mashindano ya wanafunzi kufanya miradi mbalimbali ya kijasiriamali na ubunifu na kuleta matokeo chanya kijamii.
VIGEZO MUHIMU
Mahuvi anasema, miradi hiyo inakuwa na vigezo vikubwa vitatu, kwanza kuwapa nafasi ya kujitambua na kutumia uwezo wao, ambao mara nyingi hauonekani kwa urahisi.
Pili, anasema miradi hiyo inapaswa kuwapa nafasi kupata ujuzi na mwisho kuleta mabadiliko chanya katika jamii inayowazunguka ndani na nje ya shule.
Anabainisha kwamba, wanafunzi hupewa muda maalumu wa kufanya miradi hiyo kwa miezi sita na kila wanaofanikiwa hupata tuzo kwa madaraja matatu.
Mahuvi anasema, tangu mradi kuanza umewafikia wanafunzi 12,000 kutoka shule mbalimbali katika Uwezo Award, iianzia mwaka 2016.
Mratibu huyo anataja waliofikiwa ni shule za msingi na sekondari zaidi ya 620 za mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Anataja miradi ya kijasiriamali, pia imekuwa ikileta mabadiliko kwa jamii shuleni, wanafunzi wamefanya mambo mengi kuboresha mazingira ya shule yao.
Mahuvi anataja hadi sasa kuna miradi minne, akiitaja kwa majina: Uwezo Award, Uwezo Bonanza, Uwezo Kinara na Uwezo Klabu.
“Shule zaidi ya 1300 tumezifikia tangu mwaka 2016, ujuzi wa kijasiriamali tumewapa. Kuna namna ukiwafundisha wanafunzi kazi za nje za darasa tunaleta athari chanya za ajira.
“Tulifanya survey (utafiti mdogo) kwa wanafunzi 500 ambao waliwahi kupita katika mradi huu, ambao wapo katika soko la ajira. Zaidi ya asilimia 70 waliaminiwa katika uongozi,” anasema Mahuvi.
Anafafanua kuwa asilimia 90 ya waliowahi kuwa katika mradi huo, wamepata ujuzi wa kijasiriamali na zaidi ya nusu yao wameanzisha biashara binfasi.
“Tunatamani huu mradi uwe sehemu ya mtaala wa elimu. Haina maana mtu unamapa digrii, lakini hawezi kutumia fursa ya kujiajiri,” anaeleza Mahuvi.
MFANO SHULENI KIBITI
Pia anataja mwaka jana, Shule ya Sekondari Kibiti kutoka wilayani Kibiti mkoani Pwani, waliibuka washindi pekee wa tuzo ya dhahabu kwenye mradi wa ‘Uwezo’.
Anasema wanafunzi hao walibuni mradi wa kulima ufuta na pesa walizozipata baada ya mavuno, walikarabati majengo ya shule yao, pia kupeleka zawadi katika zahanati ya Kibiti kama vile sabuni, maji, mafuta. Pia, waliopatiwa shilingi milioni.
Mahuvi anawataja washindi wa pili, ni Shule ya Sekondari, Abdallah Ulega, wilaya Jirani ya Mkuranga, nayo mkoani Pwani, wakiibuka washindi, wakipewa Sh. 500,000,
MIKAKATI INAYOFUATA
Mahuvi anaeleza, kuwa mpango wao kwa sasa ni kuupeleka mradi kwa ngazi zote za shule za msingi, sekondari, hadi chuo kikuu.
Anasema kwa sasa wanafanya mradi huo katika mikoa miwili tu. Mbali na Pwani, Dar es Salaam wanajikita katika halmashauri tano ambazo ni Kigamboni, Ilala, Ubungo, Kinondoni, Temeke.
Anasema matarajio yao ni kupeleka katika shule za mikoa mingine, dhamira kuu ikiwa kufika nchi nzima, Tanzania Bara na Visiwani.
Mahuvi anasema, kikubwa ambacho wamejifunza hivi karibuni ni kwamba, wanafunzi na vijana kwa jumla wana uhitaji mkubwa ya kuwasaidia kukuza ujuzi na maarifa endelevu, walishinde soko la ajira.
Anasema wanakukusudia kuainisha miradi mingine ya ubunifu, itakayosaidia kuwapa nyenzo vijana wanaopitia kwao kuondoka na mawazo ya kupiga hatua ziadi, ikiwamo kuanzisha biashara.
WANAFUNZI WAFUNGUKA
Rebeca Muna, mmoja wa wanufaika wa mradi wakati akiwa shuleni, Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, anasema alikuwa akishiriki katika miradi ya Uwezo Awards kuanzia mwaka 2019hadi 202o.
Anatamka mradi umemkomaza masoko yake na amejiajiri, akikiri ni mradi uliochangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya ukuaji tangu alipokuwa binti na kiongozi wa kikundi.
Rebeca anataja mafanikio yake, amemaliza shule na ujuzi ambao ni muhimu kwake kimaisha, ikiwamo uwezo wa kuongea katika hadhara, na kutengeneza mradi.
Rebeca: “Imenisaidia kufahamika na kukutana na watu wengi, imenisaidia kuongeza wasifu wangu katika kazi. Hata katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Dunuani maka 2022 nilishiriki kupitia kuimba mashairi”.
Sasa anaeleza matarajio yake ni kuwa mfanyabiashara mkubwa Afrika na nje ya Afrika, pamoja na kuanzisha kampuni yake itakayojihusisha na kutengeneza bidhaa.
“Najiona kupiga hatua zaidi na kufika mbali. Najiona binti ambaye nitaleta maendeleo chanya kwenye taifa,” anasema Rebeca.
James Jackson, Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha, anaeleza: “Uwezo Awards imetusaidia kuwa wabunifu na wajasiriamali.
“Sisi tulishiriki katika project (miradi) ya kubuni na kutengeneza kipeperushi ambacho lilikuwa linaelezea mazingira ya shule.
“Tuliyauza katika graduation (mahafali) yetu na kupata pesa ambazo zilitusaidia kujikimu katika mahitaji yetu na pesa zingine tulizitumia kufanya miradi mingine shuleni kama vile kulima mboga”.
James anasema, sehemu ya fedha pia walizitumia kuendeleza mazingira shuleni kwa kutengeneza dustibin za kutunzia takataka shuleni.
Anasema: “Mradi wa Uwezo umetuongezea ujuzi katika taaluma, kujua baadhi ya vitu tunavyofundishwa darasani ukizingatia sisi ni wanafunzi wa mchepuo wa sayansi.”
Mwalimu kutoka Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa, Emmanuel Elibariki, anatamka: “Ni moja ya miradi inayowasaidia wanafunzi kukuza vipaji vyao kama vile wachoraji, wanamuziki, wanafunzi kujihusisha na masuala ya kijamii kama vile kutoa misaada hospitalini pamoja na watoto yatima”.
Anasema njia bora ya kumjenga mwanafunzi akiwa shuleni ni kujifunza kwa kuona na kufanya, kupitia miradi hii inawasaidia katika masomo yao kwa vitendo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED