DRC, M23 kukutana kwa mara ya kwanza Aprili 9 Doha

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:46 AM Apr 02 2025
Waasi wa M23.
Picha: Mtandao
Waasi wa M23.

Waasi wa M23 wameeleza kuwa pande zote mbili zinatarajia kufanya mazungumzo ya moja kwa moja kwa mara ya kwanza mnamo Aprili 9.

Mkutano huo, unaopangwa kufanyika mjini Doha, utakuwa wa kwanza wa aina yake tangu waasi wa M23 walipoiteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Afisa mmoja wa serikali ya DRC amethibitisha kuwa mazungumzo hayo yamepangwa kufanyika kama ilivyokubalika, isipokuwa tu iwapo kutatokea hali itakayokiuka makubaliano hayo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, pande zote mbili zimekubaliana kutojadili hadharani maudhui ya mazungumzo hayo.

Kwa sasa, DRC inakabiliwa na mojawapo ya changamoto kubwa zaidi za kibinadamu kutokana na machafuko yanayoendelea na hali ya ukosefu wa utulivu. Mamilioni ya watu tayari wamelazimika kuyahama makazi yao, huku takriban watu 7,000 wakiwa wamepoteza maisha katika miezi ya hivi karibuni.