JKT, WAZO LILILOASISIWA 1958; Kawawa alivutiwa ugenini, akamshirikisha Nyerere

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:43 PM Apr 02 2025
•	Mkuu wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele
Picha: Mtandao
• Mkuu wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele

HISTORIA ya kuanzishwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), inaanzia mwaka 1958 wakati wa ziara ya viongozi wa taifa kwenda nchini Ghana.

Mwalimu Julius Nyerere na Rashid Kawawa, walikwenda kuhudhuria sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa uhuru wa nchi hiyo.

Wakati wakiwa nchini humo, Kawawa alialikwa chakula cha jioni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Israel, Golda Meir.

Kawawa alipata fursa ya kuzungumza na kiongozi huyo, ambaye alibainisha namna taifa la Israel, linavyowaandaa vijana wake kutumikia nchi yao, kwa moyo wa uzalendo.

Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mafunzoni katika picha tofauti
Kawawa, alivutiwa na maelezo yaliyotolewa na Meir, kwa namna ya utaratibu unaotumika na Israel, kuwakusanya na kuwaandaa vijana kijeshi, baadaye kufanya majukumu mengine ya kitaifa kwa ujasiri, uvumilivu, ushirikiano na nidhamu.

Aliporejea hotelini huko Ghana, walikofikia na Mwalimu Nyerere, Kawawa alimwelezea juu ya mazungumzo yake na Meir, ambayo yalimvutia na kumwagiza ayafanyie kazi watakaporejea nchini.

Waliporejea nchini, Kawawa aliyawasilisha mawazo hayo kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha TANU (TYL), Joseph Nyerere, akisaidiwa na Nangwanda Lawi Sijaona. 

Viongozi hao kwa pamoja, waliafiki mawazo hayo na kuyapeleka katika Mkutano Mkuu wa TYL, uliofanyika Tabora, Agosti 25, 1958, ili kujadiliwa zaidi na wajumbe.

Hata hivyo, mkutano wa TANU ulishindwa kuidhinisha uanzishwaji wa mafunzo hayo, kwa kuwa Tanganyika ilikuwa inatawaliwa na Uingereza chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa (UNO). 

Baada ya Uhuru wa Tanganyika, Desemba 9, 1961 wazo hilo liliwasilishwa kwa mara ya pili, kwenye Mkutano Mkuu wa Vijana wa TANU, Agosti 25, 1962 mjini Tabora.

Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mafunzoni katika picha tofauti
Mkutano huo uliazimia kutekeleza wazo la kuanzishwa rasmi kwa taasisi ya kuandaa vijana kuwajengea uzalendo na umoja wa kitaifa. 

Wajumbe wa kikao hicho walikuwa Joseph Nyerere (Mbunge na Katibu Mkuu TYL); Isack Malecela (Katibu Mkuu wa Mambo ya Fedha TYL); Moses Nnauye; H.S.J Zingaro (Katibu Mkuu Mtendaji TYL) na Meja Yaffer Ben Amots wa Israel (mshauri mtaalamu wa mpango huo).

Baada ya mkutano huo, mapendekezo ya kuanzishwa chombo rasmi cha kitaifa cha kuandaa vijana kuwa wazalendo, yaliwasilishwa serikalini na kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri, Aprili 1963.

Serikali iliridhia chombo hicho kiitwe Jeshi la Kujenga Taifa, chini ya Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. 

Wizara hiyo iliongozwa na Waziri Nangwanda Sijaona, (Mwenyekiti TYL); Joseph Nyerere (Naibu Waziri na Katibu TYL) na Mzee Harubu Saidi (Katibu Mkuu wa Wizara).

Mnamo Julai 10, 1963 JKT ilianzishwa rasmi, bila kutungwa sheria na Bunge la Tanganyika.

SHERIA YA JKT

JKT ilianzishwa kwa Sheria Namba 16 (National Service Act, 1964), iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002 kifungu 3(1). 

Sheria hiyo ilipitishwa kuwataka vijana kujitolea kwa hiari kujiunga na JKT, ili kulitumikia taifa. 

Vijana hao walitakiwa kuwa angalau wawe wamehitimu elimu ya msingi, yaani darasa la saba, wanachama wa TYL, wasiwe wameoa au kuolewa na wawe tayari kujitolea kutumikia taifa kwa muda wa miaka miwili. 

Baada ya kupitishwa sheria hiyo, Novemba, 1964 kundi la kwanza liliripoti kambi ya Mgulani JKT na kuitwa Operesheni Maendeleo, likiwa na vijana 486.

MAFUNZO JKT KUREJEA

Kurejeshwa kwa mafunzo ya JKT, kwa mujibu wa sheria ilikuwa ni moja ya mambo yaliyopewa kipaumbele cha juu katika awamu ya nne ya serikali ya Amiri Jeshi Mkuu na Rais Jakaya Kikwete. 

Serikali ya awamu ya nne, ilirudisha mafunzo ya JKT kwa sababu ya nia njema ya kuendelea kujenga uzalendo kwa vijana wa Tanzania. 

Itakumbukwa kwamba kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, serikali ilishindwa kumudu kuendesha mafunzo ya JKT kwa mujibu. 

Juni 15, 1994 mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria yalisitishwa kwa muda.

MALENGO YA JKT

Jeshi la Kujenga Taifa, limefanya kazi ya kujenga moyo wa utaifa na uzalendo miongoni mwa vijana waliopitia katika jeshi hilo, ikiwa ni sehemu ya malengo yake. 

Hapa ni mahali vijana wa itikadi zote, rangi zote, makabila yote, dini zote hukutana, kuishi pamoja na kufanya mafunzo na kazi kama ndugu wa familia moja.

Hakuna chombo chochote cha malezi ya vijana kilichoizidi JKT katika kazi hiyo, pengine hata ile tabia ya Watanzania wengi kutoulizana makabila yao inatokana na uwapo wa JKT. 

Vijana wazalendo wa Tanzania wanaopitia JKT, huwa wanakutana na vijana mbalimbali kutoka kila kona ya nchi, ndiyo maana hawana muda hata wa kuulizana makabila kwa vile wote hujiona ni wamoja.

Aidha, athari za kusimamishwa kwa mafunzo ya JKT kuliwagusa wengi na ndiyo maana serikali ya awamu ya nne ilirejesha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria. 

Hatimaye Machi 26, 2013 mafunzo ya JKT yalianza, ikiwa ni pamoja na kutimiza ahadi ya serikali ya kufufua upya mafunzo hayo katika kambi ya Ruvu.

Kama ilivyokuwa mwaka 1964, JKT ilipoanza na mwaka 1968, baada ya mafunzo ya mujibu wa sheria kuanzishwa viongozi wa kitaifa, waliongoza katika kushiriki mafunzo hayo. 

Mafunzo hayo ya JKT yalianza na kulikuwa na idadi ya wabunge 22 ambao walishiriki na kumaliza mafunzo ya uongozi. 

Wabunge hao walitawanywa katika kambi mbalimbali, kwa ajili ya mafunzo ya muda wa miezi miwili waliyoomba wenyewe, kwa ajili ya kupata mafunzo ambayo wanaamini yatawajengea uzalendo zaidi kwa taifa lao.

VIONGOZI KUJIUNGA JKT

Tangu mwaka 1968, viongozi wa kitaifa walihamasika kufanya mafunzo ya JKT. Miongoni mwao ni; Mwalimu Nyerere katika Operesheni Mwenge, JKT Mafinga mwaka 1968.

Wengine ni Aboud Jumbe Mwinyi (Makamu wa Kwanza wa Rais); Kawawa (Waziri Mkuu na Makamu wa Pili Rais); Adam Sapi Mkwawa (Spika wa Bunge); Edward Moringe Sokoine (Waziri wa Ulinzi); Job Lusinde (Waziri wa Mawasiliano); Abdulrahman Mohammed Babu (Waziri wa Mambo ya Nje) na wengineo ambao wote walipata mafunzo JKT Ruvu Operesheni Kazi ‘B’ mwaka 1968.

Pia, Benjamini Mkapa (Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Uhuru, baadaye Rais wa Tanzania), alifanya mafunzo JKT Ruvu, Operesheni Tekeleza mwaka 1971.

Benard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mstaafu), alifanya mafunzo JKT Oljoro, Operesheni Muungano (JW na JKT) mwaka 1975/76.

Aidha, Vijana wengi wa kitanzania walipata fursa ya kutumikia taifa kupitia JKT na baadaye kuwa viongozi. Miongoni mwao ni; Othman Chande (Jaji Mkuu Mstaafu) Operesheni Utii mwaka 1967; Zakhia Meghji (Waziri wa Fedha Mstaafu) Operesheni Utamaduni mwaka 1969; Fredrick Sumaye (Waziri Mkuu Mstaafu) Operesheni Mwangaza mwaka 1970.

Kadhalika Edward Lowassa (Waziri Mkuu Mstaafu) Operesheni Mikoa JKT Ruvu mwaka 1970; Mizengo Pinda (Waziri Mkuu Mstaafu) Operesheni Mikoa JKT Ruvu mwaka 1970; Dkt.Jakaya Kikwete (Rais wa Awamu ya Nne) Operesheni Tumaini, JKT Ruvu, mwaka 1972.

Pia, Jenerali Salvatory Venance Mabeyo (Mkuu wa Majeshi Mstaafu) Operesheni Usafi, JKT Mafinga, mwaka 1978; Meja Jenerali Michael Isamuhyo (baadaye alikuwa Mkuu wa JKT) Operesheni Mazoezi JKT Ruvu, mwaka 1978; Dk. John Magufuli (Rais wa awamu ya Tano) Operesheni Mshikimano JKT Makutupora mwaka 1984.

Wamo pia Jenista Mhagama (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu) Operesheni Kambarage JKT Mlale mwaka 1990/91; Meja Jenerali Rajabu Mabele (Mkuu wa JKT) Operesheni Kambarage JKT Ruvu mwaka 1990/91 na Jenerali Jacob Mkunda (Mkuu wa Majeshi) Operesheni Vyama Vingi, JKT Ruvu mwaka 1992.

WAKUU WA JKT

Wakuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), tangu kuanzishwa kwake mwaka 1963 ni takribani 15 ambao ni; ASP David Nkulila (1963-1967); ASP Robert Kaswende (1967-1970); ASP Laurence Gama (1970-1973); Meja Jenerali Nelson Mkisi (1973-1989) 

Meja Jenerali Makame Rashidi (1989-2001); Meja Jenerali Davis Mwamunyange (2001-2006); Meja Jenerali Abdulrahman Shimbo (2006-2007); Meja Jenerali Martin Madata (2007-2008) na Meja Jenerali Samwel Kitundu (2008-2012).

Luteni Jenerali Samweli Ndomba (2012-2012); Meja Jenerali Raphael Muhuga (2012-2016); Meja Jenerali Michael Isamuhyo (2016-2019); Meja Jenerali Martin Busungu (2018-2019); Brigedia Jenerali Charles Mbuge (2019-2021); Meja Jenerali Rajabu Mabele (2021-hadi sasa).

   Kwa mujibu wa tovuti ya JKT