Kuenea minara ya mawasiliano ya simu za mkononi na mitambo ya kurushia mawimbi vimewezesha laini zinazotumika nchini kuongezeka kwa asilimia 35 na kwa asilimia 41 kwenye mikoa minne ndani ya miezi 18, kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za mawasiliano.
Ripoti ya Hali ya Mawasiliano Tanzania kati ya Januari na Machi 2025 iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonesha kuwa usajili wa laini za simu uliongezeka kwa asilimia 41 mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na Tanga kati ya Septemba 2023 na Machi mwaka huu.
Aidha, serikali inakamilisha ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu 758 na kuboresha mingine 300 nchini kote, ili iwezesha utoaji huduma kwa teknolojia ya uzao wa tatu, wa nne na wa tano wa mawasiliano ya simu kwa vifaa vya mkononi (3G,4G na 5G).
Ripoti hiyo, iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari inasema laini 67,024,338 zilisajiliwa nchini kote hadi Septemba 2023 na 90,298,941 kufikia Machi 2025.
“Ongezeko la laini kati ya Septemba 2023 na Machi mwaka huu kwenye mikoa hiyo minne, na idadi kwenye mabano ni: Kagera (1,577,159 hadi 2,224,115), Kigoma (kutoka 1,279,021 mpaka 1,803,679), Tabora (kutoka 3,099,517 kufikia 4,371,032) na Tanga kutoka 2,365,189 hadi 3,335,396,”imefafanuliwa kwenye hiyo ripoti.
Aidha, imeonyesha mikoa hiyo pia ni miongoni mwa 12 yenye idadi kubwa ya mitambo inayowezesha mawasiliano ya 4G.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, teknolojia za juu zaidi za mawasiliano ya simu za mkononi yanaimarisha ubora wa maongezi na kuongeza kasi ya kutuma na kupokea data, hivyo kukidhi matarajio ya watumiaji.
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unasimamia mradi wa ujenzi na uboreshaji minara, ulizinduliwa 13 Mei 2023 na Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, serikali imejenga minara 42 Unguja na Pemba, ambako kulikuwa na minara 9,278 Tanzania Machi 2025 kulinganisha na 8,551 in Juni 2024, ongezeko la asilimia 8.5.
Ripoti ya TCRA pia inaonesha kuwa uzao wa tano (5G) wa teknolojia ya mawasiliano kwa vifaa vya mkononi ilikuwa imeenea miongoni kwa watu kwa asilimia 23 na kijiografia nchini kwa asilimia 3.6 kufikia Machi 2025.
“Mikoa yote sasa ina angalau mnara mmoja wenye mitambo ya 5G. Mikoa iliyokuwa haina hadi Juni 2024 ni Mtwara, Lindi, Kaskazini Pemba na Katavi,”amesema Dk.Jabiri.
Aidha, ripoti hiyo imeonesha kuwa mikoa 10 inayoongoza kwa mitambo na idadi kwenye mabano ni: Dar es Salaam (633), Mjini Magharibi Zanzibar (60), Dodoma (46), Mwanza (41), Arusha (34), Mbeya (16), Songwe (13) Morogoro (9), Pwani (9) na Kilimanjaro (8).
Mkurugenzi huyo amesema teknolojia ya 5G iliingia Tanzania Septemba 2022, na kwamba ina ufanisi zaidi na inawezesha mifumo na program tumizi zinazohitaji kasi kubwa ya data mitandaoni na ambayo inaunganisha na kuwezesha kutumika vifaa vingi kwa mara moja.
Vile vile, hadi Machi 2025 teknolojia zilienea miongoni mwa watu kama ifuatavyo: uzao wa pili (2G) asilimia 98.4, 3G asilimia 92.2, 4G asilimia 90.7 na 5G asilimia 23, na kwamba kuenea kijiografia kulikuwa asilimia 76.2, 74.3, 73.3 na 3.6, mtawalia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED