Mkuu wa Jeshi la Myanmar amekataa mapendekezo ya kusitisha mapigano kutoka kwa makundi ya waasi ili kuwezesha shughuli za uokoaji na utoaji wa misaada katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi.
Serikali kivuli iliyoundwa na wabunge walioondolewa katika mapinduzi ya kijeshi ya 2021 ilikuwa imetangaza kusitisha mapigano kwa wiki mbili siku ya Jumapili, ikisema kuwa miundombinu duni na migogoro inatatiza sana juhudi za kutoa misaada.
Hata hivyo mkuu wa junta Min Aung Hlaing ameshutumu makundi yanayoshirikiana na serikali kivuli kwa kutumia vibaya usitishaji wa mapigano .
"Baadhi ya makabila yenye silaha yanaweza yasishiriki kikamilifu katika vita hivi sasa, lakini yanakusanyika na kufanya mazoezi ili kujiandaa kwa mashambulizi. "
Kwa kuwa hii ni aina ya uchokozi, jeshi litaendelea na operesheni muhimu za ulinzi," alisema wakati wa hafla ya kuchangisha pesa katika mji mkuu wa Nay Pyi Taw siku ya Jumanne.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani, jeshi limeendeleza mashambulizi yake kote nchini katika siku chache zilizopita, ikiwa ni pamoja na kufyatua risasi kwenye vijiji vya eneo lililokumbwa na tetemeko hilo.
Chanzo: BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED