KATIKA historia ya siasa duniani hufanikishwa na kada tofauti katika jamii. Makundi makuu huwa ni wazee, pia kinamama na vijana, ambao wana asili ya ubia wa ’mama na mtoto’.
Hata hivyo, katika uendeshaji siasa za hivi sasa, kuna makundi kadhaa mengine kama ya wanafunzi na mjumuiko wa vijiwe vya umma kama bodaboda, huwa na nafasi zao.
Wanapotajwa vijana, wamo katika historia ya kuchangamsha na hata kufanikisha siasa, huku wakijumuisha makundi yote mawili ya kijinsia.
Katika historia nchini, vijana mara zote wamebeba nafasi kama watendaji wakuu wa siasa. Hiyo inajipa ushuhuda hata katika utafutaji uhuru wa nchini, Julius Nyerere (32) na rafikiye Rashid Kawawa, (28).
Wote walikuwa vijana, Nyerere na TANU, huku Kawawa akipambana na chama cha wafanyakazi TFL, katika ubia wa siri wakawa na nyendo za kusaka uhuru.
Leo hii klabu ya soka ya Young Africans Sports Club (Yanga), inajigamba kuwa “Klabu ya Wananchi”, chimbuko lake narejea mazungumzo yangu na Mama Maria Nyerere, kijijini Butiama, sasa yatimu miongo miwili.
Akafafanua namna kada Joseph Nyerere, mdogo wa Mwalimu Nyerere, akiwa mratibu wa nyendo za vijana wa TANU katika kuisaka uhuru alitumia kwa siri ngome ya Yanga, Mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam, kufanikisha uhuru wananchi uliopatikana mwaka 1961. Maana alijua ni penye mkusanyiko wa vijana.
Hata baada ya uhuru, Joseph Nyerere akakabidhiwa jukumu la Naibu Waziri, akiwajibika na vijana maana alikuwa mzoefu nao, hata umri wake alilingana nao.
HISTORIA JIRANI
Ndio ilivyo hata katika historia ya nchi jirani za Afrika Mashariki kama Uganda, kuliundwa ngome za vuguvugu la vijana kwa majina kama Young People of Toro, pia Young People of Kabarega.
Nchini Kenya vikundi kama hivyo vikianzia kwenye ukabila, mojawapo ndicho hatimaye kikaunda chama cha KANU chini ya kijana wa wakati huo, Johnston Kamau, baadaye akajulikana Jomo Kenyatta, baada ya kupatikana uhuru wao mwaka 1963.
Hata kurejewa nchini Malawi, Dk. Kamuzu Banda, kijana ambaye alienda kusaka maisha Afrika Kusini, akafanikiwa kupata elimu iliyojitosheleza, ndio akaja kuwa machachari kwao kufanikisha uhuru wa nchi yake mwaka mmoja baada ya Kenya.
Kwa ujumla wake, wanasiasa hao waliokomaa tangu ujana wao katika siasa kama vile Kenyatta na Kwame Nkurumah wa Ghana, walikuwa mfano mkubwa kumuonyesha njia mdogo wao Nyerere, alipoingia katika siasa za ukombozi, maana wao walishikamana katika nyendo zao za Afrika.
Hata leo hii nchini Afrika Kusini kuna kijana Julius Malema, mpinzani wa ANC, mwanzo wake ulikuwa kijana aliyeyelewa na chama tawala ANC.
Hilo hata likaendelezwa katika siasa za nchini baadaye, nyendo za maendeleo kitaifa, uwekezaji ukawa kwa vijana kwa namna tofauti.
Mathalan mwaka 1963 ikiwa miaka miwili baada ya uhuru, lilianzishwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), nalo likalenga kuwanoa na kuwaandaa vijana ukakamavu na uzalendo, kwa nia kushika dhamana za kujenga taifa baadaye.
Hadi kutangazwa miaka 10 ya uhuru wa nchi, kulikuwapo mabadililo makubwa. Taifa lilikuwa linatekeleza mipango ya maendeleo, awamu ya pili.
Awamu ya kwanza, mwaka 1964 hadi 1969 ilizama zaidi katika kuandaa mambo ya msingi, kama kuwa na viwanda vya kuzalisha mahitaji ya lazima ikiwamo nguo, huduma kama shule na hisopitali.
Baada ya kuwa na sura ya kujitosheleza, hatua iliyofuata ililenga kupiga hatua zaidi ya mahitaji ya msingi, kama kuwa na viwanda vya kati, vinavyozalisha bidhaa za uzalishaji na malighafi ya ziada.
Baadhi ndio zikawa viwanda vya kuzalisha vifaa vya kilimo (UFI) cha Ubungo na Kiwanda cha Kuzalisha Viwanda vya Kulimia (KIZAKU), Mbeya.
Kitaaluma vikianzishwa asasi kama Bodi ya Udhibiti na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), kwa lengo la kuboresha na kutanua mawanda ya kitaaluma, walengwa ni vijana wa Kitanzania.
Nikimrejea Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba, hadi kufika katikati ya miaka ya 1970, Rais Nyerere akaandaa dira ya kupokeza kijiti cha jukumu la taifa kwa vijana wenye ‘damu inachemka’ kuendeleza walikofika.
Hapo akashuhudiwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine wakati huo umri wake haujafika miaka 40. Mtazamo ulikuwa “kumpatia jukumu kijana anayeweza.’
Ni miaka hiyo, pia ndani ya TANU ikaja na programu ya kuchukua vijana wasomi wahitimu wa vyuo vya juu, kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakatumikia chama kwa sura ya kujitolea kwanza.
Walijengwa kwa mafunzo mbalimbali ya uzoefu na darasani kama vile kusukwa kiuongozi, ikiwamo katika Chuo cha TANU Kigamboni, Dar es Salaam, hata mafunzo ya kijeshi na majukumu mengineyo.
Mwisho wake ndio ikazaa kuibuka kwa majina makubwa kitaifa kama Luteni Kanali Jakaya, Kapteni Ditopile Mzuzuri na Kapteni George Mkuchika.
DARASA LA NCHIMBI
Hata leo kukiwapo aliyependekezwa na chama chake akitarajiwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, ni zao la kuandaliwa kwa siasa za chama hicho tangu umri mdogo wa shule.
Nikipiga hatua nyuma miongo mwili na nusu sasa, akiwa kijana asiyevuka umri miaka 30 nilivyofanya mazungumzo naye alishaiva kisiasa ‘kupindukia’ hata kumvusha kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana CCM, ikimuwezesha kuwa mjumbe wa vikao vya juu kichama.
Akanisumulia namna wakati huo baba yake anaishi na kutumikia katika Chuo cha CCM Kivukoni, wakaanza kunolewa katika umri mdogo wa shule ya msingi.
“Tulikuwa tunafundishwa ule wimbo eeh vijana!...” akanisimulia Nchimbi, akimtaja miongoni mwa waliomnoa miaka hiyo akiwa mkufunzi siasa, ni Philip Mangula, aliyewahi kushika nafasi ya sasa ya Dk. Nchimbi, Katibu Mkuu wa CCM.
Wakati anachukua nafasi ya kuongoza Umoja wa Vijana CCM, pia ndio walikuwa wanachipukia kwa makali, kada kama Amos Makalla, Katibu Mwrnezi wa CCM wote wakiwa ‘wabichi’ wamehitimu masomo yao si muda mrefu
MAGEUZI YA SIASA
Tafsiri ya nguvu za vijana, tena ikaonekana katika vuguvugu la kutaka mageuzi ya taifa kuingia katika mfumo wa vyama vingi mapema ilipoingia miaka ya 1990.
Wanasiasa mitaani kama vile kina Mabere Marando, Abdallah Fundikira, Seif Sharif Hamad, wakiungana na kundi la wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hasa kutoka Idara za Sheria na Sayansi Siasa, kama Dk. Masumbuko Lamwai, Dk. Ringo Tenga na Profesa Mwesiga Baregu.
Hao waliungana katika vuguvugu la shinikizo hilo la kisiasa kitaifa, chini ya kivuli cha chombo chao kilichoitwa National Convention for Construction and Reform (NCCR), wakiwa na uiba na wanafunzi wao wa Chuo Kikuu cha Dar es s Salaam, kama kina James Mbatia, Mosena Nyambabe ‘Ngoa Kisiki’ na Anthony Komu wakaleta mageuzi.
Hata baadaye kukaundwa Tume ya Jaji Nyalali kufanyia kazi maoni hayo, ndio mwaka 1992, Tanzania ikaingia katika vyama vingi.
Hapo vyama vikazaliwa, chombo NCCR kikibadilika kuwa chama NCCR Mageuzi, huku vijana kama Mbatia aliyepoteza masomo na Nyambabe, wakawa vigogo wa chama hicho, chini ya kina Marando.
Hata miaka saba baada ya mageuzi hayo kuidhinishwa nchini, tena utashi wa vijana kisiasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, chama Chadema kikinyakua umaarufu wa NCCR Mageuzi iliyoingia katika mpasuko.
Ndani yake ndio ikawaibua nuru inayowaka kisiasa leo kama vile kina Zitto Kabwe na Profesa Kitilia Mkumbo, hata kuhitimisha tena kuwa, vijana huwa ni mtaji muhimu katika nyendo za kisiasa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED