IMEELEZWA miongoni mwa wagonjwa wa usonji wapo ambao wenye upeo mkubwa.
Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasiyoambukiza wa Wizara ya Afya, Dk. Omary Ubuguyu, amesema wakati wa mkutano wa Maadhimisho ya Siku ya Usonji Duniani, jijini Dar es Salaam leo, ambayo hufanyikia Aprili 2 ya kila mwaka.
"Usonji kuwa ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa fahamu na ukuaji, hivyo kusababisha hali ya upekee inayohusiana na utofauti katika namna mtu anavyofikiri, wapo wanaofikiri jambo moja kwa kiwango cha juu na hata anavyojifunza na jinsi anavyohusiana na wengine,"
Hali hii pia inaweza kuambatana na magonjwa mengine ya akili na mfumo wa fahamu ikiwamo kifafa au “hali ya kukosa utulivu” (ADHD) na kwa baadhi ya wagonjwa kuwa na uwezo wa chini kabisa wa ufahamu.
Pia wapo watu wenye tatizo la usonji ambao tatizo kubwa linabaki kwenye mawasiliano na mahusiano pekee, bila ya kuonesha dalili yeyote ya ugonjwa.
"Haiwezekani kuzuia wazazi kupata mtoto mwenye usonji, ila inawezekana kuongeza uwezekano wa kupata watoto wenye afya nzuri kwa kufanya mabadiliko muhimu katika mtindo wa maisha," anasema Dk. Ubuguyu.
Amesema hiyo ni pamoja na kula mlo bora, kufanya mazoezi mara kwa mara, na kuhakikisha uchunguzi wa afya kabla na wakati wa ujauzito.
Pia, ni muhimu kushirikiana na wataalam kuhusu matumizi ya dawa na kuepuka vinywaji vyenye kileo kama pombe hasa wakati wa ujauzito kwani vinaweza kuathiri ukuaji wa mtoto na kuongeza hatari ya matatizo ya kiafya, ikiwa ni pamoja na ulemavu wa mfumo wa fahamu.
"Dalili za kwanza za usonji huonekana kabla ya mtoto kufikia umri wa miaka mitatu, na kabla ya umri huo, ni nadra kuona dalili hizi,"alisema Dk. Ubuguyu.
Naibu Waziri wa Afya Dk. Godwin Mollel, akizungumza katika mkutano huo, amewahimiza wananchi kutowanyanyapaa wenye usonji, badala yake waone umuhimu wa kuwasaidia Kwa kuwa miongoni mwao wapo wenye uwezo mkubwa wa kufanya mambo ya kipekee.
"Miongoni mwa wanaougua Usonji wapo wenye uwezo mkubwa wa ufahamu genius, hivyo tuwekeze kwa kuwahudumia vizuri wote kuna mambo mazuri ya kuvuna," amesema Dk. Mollel
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), mtoto mmoja kati ya 100 duniani anapatwa na ugonjwa huuo, huku tafiti za Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC) za mwaka 2018 zikionesha kuwa watoto wa kiume wanaathiriwa mara nne zaidi kuliko watoto wa kike.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED