CHADEMA yakomaa kuchunguza kiongozi wao kupigwa

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 04:35 PM Mar 31 2025
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche
Picha: Mtandao
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kinafuatilia kwa karibu tuhuma zinazosambazwa mitandaoni juu ya madai ya kupigwa kwa Mratibu wa Uenezi wa Baraza la Wanawake (BAWACHA), Sigrada Mligo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Brenda Rupia, kinafuatilia kila hatua inayochukuliwa kwa kushirikiana na vyombo husika vya ndani na nje ya chama.

Amesema chama hicho kitatoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo, kwa kadri itakavyofaa.

Kadhalika, chama hicho kimemtahadharisha kiongozi wake huyo wa Uenezi kuwa makini na uhusiano wake na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kuepuka kutumiwa kwa malengo yasiyo na nia njema ya kuathiri si tu hadhi ya chama hicho, bali na ya kwake pia.

Sigrada anadaiwa kupigwa Machi 25, mwaka huu , mkoani Njombe na mmoja wa walinzi wa CHADEMA  kwenye kikao cha ndani kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche.