Bonanza kuhamasisha uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru lafanyika Pwani

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:01 PM Apr 01 2025
Matukio ya bonanza la kuhamasisha wananchi kushiriki uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa.
Picha: Julieth Mkireri
Matukio ya bonanza la kuhamasisha wananchi kushiriki uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa.

Taasisi ya Bega kwa Bega mkoani Pwani imefanya bonanza la siku moja kwa lengo la kuhamasisha wananchi kushiriki uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, unaotarajiwa kufanyika kesho, Aprili 2, katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.

Mbio hizo zitazinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Isdor Mpango.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, Mratibu wa Taifa wa Taasisi hiyo, Ruth Mateleka, amesema taasisi yao inahamasisha na kuisemea miradi mbalimbali iliyotekelezwa na serikali, ili wananchi watambue maendeleo yaliyofanyika na jinsi miradi hiyo ilivyoondoa kero katika jamii.

"Taasisi yetu tayari imefika katika mikoa 12 nchini na tumeendelea kusimulia kazi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa wananchi," amesema Ruth.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mkoa wa Pwani, Zuhura Sekelela, amesema bonanza hilo limehusisha michezo mbalimbali kama kuvuta kamba, kutembea na gunia, kukimbiza kuku, mpira wa miguu, na ngoma za asili.

"Bonanza letu limelenga kuhamasisha wananchi kushiriki uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, na sisi tuko tayari kushiriki kikamilifu," amesema Zuhura.

Ameongeza kuwa taasisi hiyo pia imekuwa ikitangaza kazi za serikali, kushiriki katika shughuli za usafi wa mazingira, na kupanda miti katika maeneo mbalimbali mkoani Pwani, ikiwemo mashuleni na hospitalini.

Uchangiaji damu waupokelewa kwa hamasa kubwa

Balozi wa Taasisi hiyo, Happiness Ruta, amesema kuwa mbali na michezo, bonanza hilo lilihusisha pia zoezi la uchangiaji damu, ambapo jumla ya chupa 19 za damu zilipatikana kusaidia hospitali zinazohitaji.

Mchungaji Levalent Mwasulama, mmoja wa washiriki wa bonanza hilo, amesema amejiunga na taasisi hiyo baada ya kuvutiwa na shughuli zake, hasa katika kutangaza na kusimamia miradi ya maendeleo kwa jamii.

Maandalizi ya uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru yamekamilika

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru yamekamilika kwa asilimia 100, na kila kitu kiko tayari kwa tukio hilo kubwa la kitaifa.

Mbio za Mwenge wa Uhuru ni sehemu ya harakati za kitaifa zinazolenga kuhamasisha maendeleo, mshikamano, na uzalendo miongoni mwa Watanzania.