KOCHA Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, amewatoa hofu mashabiki wa soka mkoani Lindi akisema timu hiyo haitoshuka daraja, badala yake watapambana kuhakikisha inasalia Ligi Kuu.
Akizungumzia maendeleo ya timu hiyo, alisema ni kweli si mazuri kwa kuwa haipo kwenye eneo salama, lakini ataendelea kupambana na kuwahimiza wachezaji wake nini cha kufanya kuhakikisha mashabiki wa Lindi wanaiona tena Ligi Kuu msimu ujao.
Mgunda, ambaye ameichukua timu katikati ya ligi kutoka kwa Mwinyi Zahera, amekiongoza kikosi hicho kushinda michezo minne na sare, ikipata vipigo saba kwenye michezo 16 aliyoiongoza.
“Ni kweli hatupo vizuri sana, lakini matatizo hayakimbiwi bali yanatatuliwa. Nimeongea sana na wachezaji wangu, naamini tunakuwa bora kwenye mechi saba zilizobaki ambazo tunakutana na timu zote ambazo pia zinahitaji matokeo mazuri, naamini tutafanya vyema," alisema Mgunda, straika wa zamani wa Coastal Union.
Alisema kuwa kwa sababu ligi inakwenda ukingoni wakiwa wamesalia na michezo saba tu, watahakikisha wanafanya vizuri ili kufanikiwa lengo la kuibakisha Ligi Kuu.
Namungo inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 23, nafasi ambayo kama ikiendelea kubaki hapo, inaweza kujikuta ikishuka daraja au kwenda kucheza mechi za mchujo.
Timu hiyo kesho itajitupa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kucheza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, mzunguko wa 23 dhidi ya Pamba Jiji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED