Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, ameishukuru Italia kwa kutoa dhamana ya mkopo wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora, ambayo tayari imekamilika na imeanza kutoa huduma kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Akizungumza mjini Rome, Italia, baada ya kukutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Italia (SACE), Alessandra Ricci, Dk. Nchemba alisema huduma ya treni hiyo imepunguza muda wa safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma kutoka saa nane hadi takriban saa tatu.
Aidha, aliipongeza SACE kwa nia yake ya kuendelea kudhamini ujenzi wa reli kutoka Dodoma hadi Isaka, huku akiwaalika wawekezaji wa Italia kuwekeza Tanzania katika sekta za miundombinu na viwanda.
Kwa upande wake, Ricci alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi 14 za Afrika zitakazonufaika na usaidizi wa kifedha wa Italia kupitia Mpango wa Ushirikiano wa Piano Mattei. Aliahidi kuwa SACE itaendelea kushirikiana na Tanzania kugharamia vipande vya reli vinavyounganisha Makutupora, Tabora na Isaka ili kuimarisha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na SADC.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED