Rais Samia awakumbuka watoto yatima

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 04:04 PM Mar 31 2025
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akizungumza na watoto wanaolelewa katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Mvuma, kilichopo Kata ya Nyasubi, manispaa ya Kahama, leo
Picha: Shaban Njia
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akizungumza na watoto wanaolelewa katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Mvuma, kilichopo Kata ya Nyasubi, manispaa ya Kahama, leo

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa sadaka ya mahitaji mbalimbali, kwa watoto yatima na wanaotoka katika mazingira magumu wapatao 227, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, kwa vitu vyenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni tano.

Lengo ni kusherehekea kwa pamoja sikukuu ya Eid-Al-Fitri.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akikabidhi mbuzi
Watoto hao wanatoka katika vituo vya kulelea yatima vya Mvuma kata ya Nyasubi, Zaqalinah Kata ya Kagongwa; New Hope mtaa wa Mwime Kata ya Zongomela pamoja na Kituo cha Kahama Peace kilichopo mtaa wa Dodoma Kata ya Zongema, manispaa ya Kahama.

Aidha vituo vilivyotolewa ni pamoja na mafuta ya kula ndoo 10, sukari kilo 200, sabuni mifuko 10, maji katoni 50, juisi katoni 96, mchele kilo 50 pamoja na mbuzi 10.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, akipika chakula cha watoto yatima wanaolelewa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Mvuma, kilichopo kata ya Nyasubi, manispaa ya Kahama, baada ya kukabidhi sadaka ya mahitaji mbalimbali, iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, akikabidhi msaada huo leo, Machi 31, 2025, amesema, kila mzazi au mlezi anawajibu wa kuhakikisha analea katika misingi mizuri, kuondoa wimbi la watoto mitaani na wengi hukimbia familia zao, kwa sababu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Amesema kila mwaka Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa akila sikukuu pamoja na watoto yatima, wajane na wanaotoka katika mazingira magumu, kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali na muhimu na kuwataka wengine kufanya hivyo.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha (kulia) akishirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita (kushoto), kukata kutoweo
Ofisa Ustawi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Swaiba Chemchem, amesema watoto 227 wamefikiwa na sadaka kati yao 35 wanatoka kituo cha Mvuma, 32 Zaqalinag, 75 New Hope pamoja na 85 Kahama Peace.

Pia amesema, kituo cha New Hope kimekuwa kikipokea watoto wengi kutoka Msalala, Ushetu na manispaa hiyo, wakiwamo wanaotoka nchi jirani ya Burundi, ambao baadae wanarejeshwa nchini mwao.

Picha ya pamoja ya watoto yatima na viongozi mbalimbali wa wilaya na mkoa wa Shinyanga
Akizungumza kwa niaba ya wamiliki wa vituo hivyo, Mkurungezi wa New Hope, Suleimani Nkanda, amemshukuru Rais Samia, kwa mahitaji hayo na kuahidi kutumika kwenye matumizi yaliyopangwa.