MHANDISI NDEGE AJAYE; Binti kutoka famila duni atimiza ndoto yake

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 03:00 PM Apr 01 2025
•	Arafa Hashimu akiwa na wazazi wake, Pili Mohamed (kushoto) na  Hashimu Mazige (kulia), jijini  Dar es Salaam katika hafla ya binti  huyo kukabidhiwa ufadhili wa masomo nchini India.
Picha: Christina Mwakangale
• Arafa Hashimu akiwa na wazazi wake, Pili Mohamed (kushoto) na Hashimu Mazige (kulia), jijini Dar es Salaam katika hafla ya binti huyo kukabidhiwa ufadhili wa masomo nchini India.

UNAPOZUNGUMZA na mabinti wawili, Arafa na Latifa na wazazi wao, Hashimu, Mazige na mama yao, Pili Mohamed, ukiwakagua wanasafiri katika staili kila mmoja kumpigania mwenzake.

Kamwe hakuna anayekubali mmoja wao kubaki nyuma. kwa sasa, Latifa ambaye ni dada wa Arafa ni Mfamasia aliye masomoni, huku mdogo wake Arafa, ni Mhandisi mtarajiwa. 

Ila wazazi wao hawakupata elimu ya juu, huku baba yake ana ufundi wa kujifunza mtaani.

Mama yao, Pili Mohamed, ndiye mlezi wa familia na mkuu wa familia, baba wa wawili hao wanasanyansi, Mzee Hashimu, mwishoni mwa wiki iliyopita, alikuwa na simulizi kuhusu maendeleo ya mabinti zake, akiwa ‘baba shujaa’ dhidi ya dhana ngumu ya kusomesha mabinti ‘kihivyo’.

Hashimu Mazige na mwanawe, Arafa, nje ya nyumba yao, Mvomero mkoani Morogoro.
Hiyo ni katika tukio, familia hiyo, wakazi wa Kibati, wilayani Mvomero, mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki walifika Dar es Salaam, wakati Arafa akikabidhiwa ufadhili wa masomo na wadau wa elimu ya juu, kwenda nchini India.

MHANDISI NDEGE AJAYE

Arafa (21), anatamka ameanza masomo ya awali na elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Kibati.  

Unapozungumza naye, hafichi taswira ya usomi wake, namna anavyomudu lugha yake ya kusomea kiingereza, katika kila sentensi saba au nane, haachi kutupia neno kwa lugha hiyo yenye jina ‘ung’eng’e’ 

Arafa, anasimulia tangu awali alikotoka, namna mzazi wake alivyomhamisha shule kadhaa, na darasa la pili, baba yake (Mzee Hashimu), akamhamishia shule ya bweni inayoitwa Kirinjiko Islamic.

“Nikiwa na miaka nane, nikaanza darasa la kwanza tena mwaka 2012 katika shule ya Kirinjiko Islamic.

“Nikiwa darasa la tatu, niliwahi kuwa na ndoto ya kuwa mwanasayari, ila nilivyoendelea kukua wengi wakawa wananiambia ni ghali sana, nikaanza kuwaza basi niwe daktari.

“Kirinjiko ipo mkoa wa Kilimanjaro. Nikahitimu darasa la saba Kirinjiko Islamic, na ‘form one’ (kidato cha kwanza), nikaanza kusoma hapo hapo,” anasimulia Arafa.

Ingawa anasema kwamba, baada ya muda mfupi shuleni hapo kulifanyika mabadiliko ya ada, ilipoongezwa ikawa changamoto kwa familia yake.

“Wazazi wangu wakapata changamoto katika kulipa ada maana tulikuwa tupo wawili, mimi na dada yangu, Latifa.

“Tulipofika ‘form two’ (kidato cha pili), tukarudishwa nyumbani kwa ajili ya ada, hivyo baba yangu ikabidi atutafutie shule nyingine tukasome kwa kipindi kifupi, halafu Kirinjiko Islamic turudi kufanya mtihani wa taifa tu.

“Maana tulishasajiliwa kufanyia pale Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili. Kwa hiyo tukahamia katika shule ya bweni nyingine inayoitwa ‘At taaun Girls Seminary’, ambayo ipo Morogoro, tukasoma kidato cha pili lakini mtihani wa taifa tukafanyia Kirinjiko Islamic.

“Kisha tukarudi ‘At taaun Girls’ tena tukasoma ‘form three’ na ‘form four’ tukamalizia hapo,” anasimulia binti huyo Arafa. 

Anasema, kwa upande wa masomo ya sayansi alikuwa yupo vizuri kuanzia darasa la pili, aliyapenda sana hasa hesabu, sayansi na somo la jiografia.  

Arafa anasimulia kuwa alipofika kidato cha kwanza, alikuwa anafanya vizuri sana katika masomo ya Kemia na Fizikia. 

“Hata nilipokwenda kidato cha tano, sita nikachukua tahasusi ya ‘PGM’ katika shule ya serikali, Makambako Sekondari mkoani Njombe.

“Kidato cha tano na cha sita, masomo yalikuwa magumu, lakini niliamua kupambana nayo hivyo hivyo, kwa ajili ndoto yangu ilikuwa inanibidi nisome PGM.

“Nikasoma PGM na mpaka namaliza kidato cha sita nilikiwa na ufaulu wa Division ‘one’ ya ‘saba’ (daraja la kwanza pointi saba),” anaeleza.

CORONA ILIVYOMPA DARASA

Arafa anasema, wakati wa janga la maradhi ya Uviko 19 kuingia, shule zikilazimika kuwarudisha wanafunzi majumbani kwao, kwa takribani likizo ya miezi mitatu, kwake ilikuwa fursa ya kuimarisha anachoota.

“Ilikuwa ndoto yangu kuwa hivi nilivyo, tangu kipindi corona tuliporudishwa nyumbani, baba yangu mimi ni mbunifu anapenda kugundua vitu. Amebarikiwa hivyo.

“Baba kaishia darasa saba, yeye ni mfanyabiashara. Kipindi narudi nyumbani, nilikuwa nafikiria kuwa daktari. Ila niliporudi nyumbani baba katika teknolojia yupo vizuri hajasoma, lakini akifanya shughuli zake pale nyumbani namwangalia.

“Nilishuhudia gari ambayo ilikaa miaka mitatu pale nyumbani na mafundi wengi walishindwa, akafungua na kuishusha injini, akatuita na mimi nilikuwapo.  

“Anamaliza namwangalia, ikawaka, nikajiuliza ‘if my father can… (kana baba yangu anaweza) kwanini mimi nishindwe?

“After all (katika vyote), niliwahi ku-dream (kuota) kuwa ‘astronomist’ (mwanasayari). Halafu kila niliyekutana naye kwa mara ya kwanza aliniambia ni ghali.

“Ila niliposhuhudia wakati wa corona, nikaamua nibaki hapa hapa kuwa ‘engineer’ (mhandisi) katika ndege,” anasema.

JITIHADA ZILIVYOMBEBA

Arafa hasiti kuweka wazi undani wa jitihada zake kuna watu nyuma yake, familia kwa ujumla, wanajamii wakiwamo wadau wa elimu.

“Sisi kwetu, familia tunauza hizi barafu ‘ice cream’ za kutengeneza wenyewe. Namsaidia mama yangu kutengeneza kisha, anazichukua kwenda kuuza, unawapa hata wengine wakakuuzie.

“Nikawa naamua naweka katika ndoo kubwa naenda nazo shuleni. Kwa hiyo, nilikuwa natoka mbali, hadi shule ya sekondari kuuza barafu, unavuka vilima, unawauzia muda wa mchana labda saa nane, ukiuza sana umepata shilingi. 8,000.

“Ila siku moja niliporudi nyumbani kutoka kuuza barafu, nikamkabidhi mama mauzo, baba akasema ‘UNI AID’ (shirika la kimataifa) wamepiga simu, wanasema ulikuwa hupatikani ‘WhatsApp’. Sikutarajia kwamba nimepata ufadhili.

“Nilidhani itakuwa mwakani, nilishangazwa ‘for sure’ (kwa hakika).” anaeleza msomi huyo mwanasayansi. Naahidi kugundua vyangu yaani, kwenda mbali ya kile ninachofundishwa na wahadhiri.

“Angalau kufika mwaka wa pili niwe nimegundua kitu. Sipendi kuegemea elimu ambayo mwingine kagundua, hapo inakuwa kama mwanzo tu.

“Na nitakapomaliza na kupata kazi, nitasidia familia yangu, jamii kama mimi nilivyosaidiwa, leo sisi na sisi tusaidie wengine. 

“Hamna mtu anaandikiwa kufeli, kwanza fuatilia fursa, hii mitandao ya simu tuitumie vizuri, mimi nilikuwa naingia mtandaoni nikapata hii fursa, nilipoomba huu ufadhili kilichonisaidia ni mtandao kutumia kifursa.

“Nashauri wanaohitimu pia kidato cha sita, waangalie fursa, mitandao ya kijamii isiwe kuangalia sanaa na anasa zingine,” anaeleza Arafa  

BABA ASIMULIA CHANGAMOTO

Mzee Hashimu anasimulia historia  yake, akisema kwenye elimu kufikia hatua za juu, kwake ilikuwa changamoto, akaigeuza hiyo kuwa fursa kwa wanawe. 

“Mimi binafsi nilishindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosekana fedha, familia tulizotoka duni sana. Nilipoanza kutengeneza familia nililenga kutowaweka nilikopita mimi.

“Tulipotembelewa na mradi huu waliamini hivyo walipotutembelea. Nilisema nitahakikisha nawasomesha ninaowaandaa, kwa kuwa tulikuwa nyuma sana kielimu hata jamii inayotuzunguka. 

“Nikasema familia nitakayoitengeneza na kubahatika kupata watoto wawili, wa kwanza Latifa, kisha wa pili Arafa, nitawasomesha, Mimi mfanyabiashara mdogo.

“Nikasema kama sijasoma, nitasomesha na nikajilazimiasha kuwapeleka watoto ‘English Medium’ (shule ya kiingereza). 

“Ila mwaka 2018 nikapata ajali nikavunjika mguu. Nilikaa Muhimbili miezi mitatu, kile kipato kikaishia kwenye tiba. Ikabidi hawa watoto warudi shule za kawaida.

“Badaaye nikawapeleleka Kirinjiko, ila ikawa ada kubwa, nikampunguza mmoja, amalize kwanza mkubwa Latifa. Maana ada ilifikia shilingi. milioni mbili kwa mmoja. Kisha nikakusanya pesa Arafa anaye akaingia shule hiyo hiyo.

“Nilikutana na changamoto wengine wasomi na wasio wasomi wakisema kusomesha watoto wa kike ni hasara, hawatofika popote.

“Jamii ipo hivyo, kwamba usisomeshe, wengine wafanyakazi wa benki, ofisa mkubwa wanasema unakopa usomeshe, tunapoteza gharama, utasomesha anaishia mtaani. Nikawauliza je, nyie mlipata kazi bila kusoma?

“Nilifanya kazi kwa bosi hata kwa kudhalilika nipate ada, hata mdogo wangu pia nilimsomesha. Latifa alipomaliza kidato cha nne, akasema baba nikusaidie niende moja kwa moja chuo kusoma ufamasia.

“Ila mwaka uliofuata nikafeli ada. Akakaa nyumbani, akarudi tena, angehitimu mwaka jana ila atahitimu mwaka huu.

“Arafa akamaliza Makambako Girls, nikawa nahangaika ada nimtafutie akasome chuo. Mimi huwa natengeneza vyuma vyuma hivi naweza kubuni mashine ikafua umeme, ikapandisha maji. Sina elimu tu rasmi ila naweza.

“Si ujanja wetu ni Mungu! Nilipowapeleka watoto shule hawakuniangusha, ila niliwajenga tusaidiane. 

“Mimi nilikuwa na hali ngumu kiuchumi ila nimesaidia. Kuna familia moja ambayo walikuwa ni vipofu mtoto wao alisoma na Arafa, nilimsaidia pia. 

“Kwao huyo mtoto ni Kigoma, anasimulia kwao wote saba ni vipofu baba, yao alifariki. Na yeye ndio wa saba anaona.

“Kwa hiyo wale wa juu wote wanamwangilia huyo mdogo asome angalau aje awasaidie. Nilimsaidia niwezavyo. Kwa mwanangu Arafa, kwa hatua hii aliyofikia, akumbuke nyuma kusaidia wengine,” anasema

 Pili Mohamed, mama mzazi wa Arafa, anasema anawashukuru wadau wa elimu kumwibua mwanawe, hadi kwenda masomoni.

“Mimi kama mama nilisema sidhani kama mwanangu atasoma kile alichofaulu. Kipato chetu kidogo, namshukuru Mungu kwa hili. Namuonya Arafa, kukumbuka huko tulikotoka.

BABA ALIVYOWAJENGA MABINTI 

Hashimu anasema kwamba, mwanawe kupata fursa hiyo alitarajia ipo siku, kwa kuwa alijitajidi kuwasomesha hata shule za binafsi kulipia ikiwa ni msingi.

“Nimewajenga kuwa na fikra za kufikiri vikubwa, kuna wanaenda mpaka anga za mbali kama NASA, mtu yeyote anaweza akawa mtu mkubwa na kufanya makubwa. Haijalishi katokea shamba, kijijini.

“Mtu yeyote akiamua na kutetea muda wake anafikia mafanikio. Niliwajenga kwa kuchukuliwa mifano mingi. 

“Mfano Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ametokea kijijini Butiama, ameongoza watu ambao wako katika miji mkubwa Dar es Salaam.

“Au hata Benjamin Mkapa, ametokea Masasi, Mtwara, akaongoza Tanzania, wapo waliozaliwa mjini kama Dar es Salaam, lakini hawakuwahi kufikia hatua zake.

“Nimewajenga kimaadli hata mtandaoni nawaambia waangalie fursa. Wazazi wawajenge watoto wakiwa bado wadogo, kisaikolojia watakua hivyo hivyo. Ukikaa naye sana mbali atakosa mwelekeo. Tuzungumze nao,” anasema Hashimu.

WADAU WAWEZESHAJI 

Aloyce Mkwizu, ni Meneja Masoko kutokaUNI AID Africa, anasema lengo ni kuwasaidia wasichana kusoma kozi za sayansi na kwamba Arafa ndiye wa kwanza katika mradi huo, katika hatua ya kukamilisha idadi ya mabinti 1,000.

“Mwaka huu Arafa amepata ufadhili wa kwenda kusoma uhandisi wa ndege, nchini India, katika Chuo cha Jain.

“Tunapata ushirikiano kutoka serikalini, namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni nilitembelewa na mtu kutoka Wizara ya Elimu na kufikisha wazi hili la kuwasaidia watoto wa kike kielimu.

“Wito ni tuwe na ushirikiano wengi, wanahitaji, kwa sababu wanafunzi kwenda kusoma nje inaokoa gharama kwa Bodi ya Mikopo.

“Wazazi wawaruhuau wasichana kusoma kozi za sayansi. Jarida tulilolitoa kuhusu kufadhili mabinti wa hapa nchini, limebeba ufadhili unaofikia dola (za Marekani) 200,000. 

“Arafa atasoma kwa miaka minne ada ni dola 20,000 wastani wa Sh. milioni 40, ataondoka nchini wiki ijayo (wiki hii),” anasema.