KUEGEMEA TUISHENI KUNAVYOZALISHA, WASOMI WALIOKARIRI SI KUELEWA

By Peter Orwa , Nipashe
Published at 03:11 PM Apr 01 2025
Madarasa ya tuisheni yakiendelea
Picha: Mtandao
Madarasa ya tuisheni yakiendelea

KATIKA mada zilizopita kwa safu hii ziligusa suala la utashi wa masomo ya ziada kwa maana ya tuisheni, yalivyokuwa na athari katika uwezo wa wanafunzi shuleni.

Kupitia kikao cha mjumuiko wa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1998 (alumni convocation), wakaja na malalamiko kwamba kasoro zisizo za kawaida wanaziona masomoni.

Wajumbe wawili wanazuoni wakatoa maoni yao kwamba walibaini kuwa ‘kizazi cha tuisheni’ kimeanza kuingia masomoni katika vyuo vikuu.

Kwa mzizi wake, msingi wa tuisheni unaanzia katika zama baada ya mageuzi ya kisera nchini mwaka 1985, nchi iliporejea katika uchumi huria, baada ya kufunga milango hiyo mwaka 1964.

Katika hisabati ya miaka 13, ni mwanafunzi aliyesoma darasa la kwanza mwaka 1985 hadi kumaliza kidato cha sita, mwaka 1998 anapiga hodi chuo kikuu.

Tangu kuanza kwa mtindo huo, ukaibuka kuwa mfumo uliojenga tabia ya kimasomo wanafunzi hasa katika kipindi cha likizo wanaenda katika sehemu kunakotolewa masomo ya ziada, kwa jina ‘tuisheni’

Ndani ya muda mfupi, tabia hiyo ikakomaa na kuenea hadi shuleni kukimea madarasa hayo, huku wenye kada ya ualimu makazini shuleni, hata ukawa mtindo wa kupata fedha za ziada, ufanisi wa awali darasani ukianza kushuka taratibu.

KASORO INAKOANZIA 

Undani wa mfumo wa tuisheni kihistoria umepitia hatua kuu mbili. Wakati unaanza, wanafunzi walisaidiwa kitaaluma kwa mada zinazowatatiza, kukiwapo madarasa ya ziada kwa malipo maalum.

Lakini baadaye, ikahamia kwa wanafunzi kunolewa kwa mada zote, ikiaminika kwa wazazi huko ndiko mtoto anasukwa vyema kuziba pengo la kilichompita darasani, hatimaye ukawa utamaduni mpya wa kujisomea kwa umma.

Staili ya ufundishaji tuisheni kwa ngazi zote za masomo, ikawa wanasukwa katika mstari wa kuelewa vyema majibu ya mtihani na namna ya kupambana na aina ya maswali tarajiwa, kila anayeenda tuisheni akionekana anapata elimu bora zaidi, ikiifanya shule hiyo kupata soko.

Mbinu ya wanafunzi huko zinazama katika kukariri maudhui mbalimbali yanayohusiana na mtihani na namna ya kufikia ufanisi wa kufaulu mtihani.

Ikifahamika mfumo wa mitihani na maswali yake yenye sura ya kujirudia, wasomi wengi waliopitia tuisheni walifaulu. Hata hivyo, wakavuka viwango hivyo vya kitaaluma, huku uwezo wao wa kujifunza na kujisomea ukibaki duni, hadi ustadi wa lugha ukashauka. 

Tuisheni hizo zikawaweka katika namna tegemezi kifikra, kukariri majibu, mbinu na stadi mbalimbali za kitaaluma, kuliko kudadavua kwa mantiki binfasi.

Kadri muda ulivyopita, kizazi cha baadaye kilichoingia masomoni katika zama ‘tuisheni imechanganya’, wakadhani ndio mfumo na mbinu wa kusoma.

Niliwahi kumuuliza sababu mwanafunzi ambaye alimaliza kidato cha sita na hakufaulu vyema, akanijibu “Sikupata tuisheni ya kutosha.” 

Muda ulipopita, baadhi ya waliosoma na kufaulu katika mtindo huo wameshakuwa walimu wa ngazi mbalimbali, kuanzia shuleni hadi vyuoni.

Katika kuwajibika kwao, wengi wamechangia kudumisha taaluma kutokana na kurejesha au kuendeleza yanayoambatana na tuisheni katika ufundishaji wao.

Wanahimiza mfumo wa kufundisha wanafunzi wanaokariri na kuvizia majibu tarajiwa ya mtihani, badala ya kuelewesha kwa upana maudhui ya wanayopaswa kujua, ili wawe wataalamu wa hiyo dhana.

Hadi sasa kuna kundi la wasomi wako hata makazini, wamesafiri wamekariri majibu ya kile wanapaswa kufahamu, lakini hawajui namna yanavyodadavuliwa kwa hatua, kufikia majibu hayo. 

Je, ni hapo wanastahili kuitwa wataalamu? Haitakuwa ajabu, kumpata daktari anayekariri ugonjwa na sifa zake, pia kanuni za kutibu, ilhali uelewa wake ukibaki mdogo katika tafsiri yake pana. Atamudu vipi kung’amua kinachomtesa mgonjwa, kama maradhi yamempata kwa njia tata? Anabaki duni katika namna kudadavua kasoro. 

Hiyo inatokana na umahiri wa mwanafunzi kuelewa kutoka ngazi moja, inategemea sana alivyokomaa ngazi ya chini. Anayesomea udaktari au ufamasia, anatakiwa pasipo shaka ameiva katika msingi wa Baiolojia na Kemia, huko shuleni.

Hivyo, usomaji tuisheni kuwa kipaumbele inamjenga msomi kutojua alichofunzwa katika tafsiri pana ya ‘kwenda kushoto au kulia’ hata anapoteza sifa ya mtaalamu anayekuwa na uwezo wa kitafiti kitaaluma, ambayo msingi yake inaanzia darasani.   

NAMNA YA KUJIFUNZA

Hadi sasa, ikifuatiliwa mitaala ya kitaifa imeweka misingi ambayo mwanafuzi anapaswa kujifunza kufuata ngazi kadhaa, hadi anakomaa kwa ngazi ya juu.

Namna ya kupitia ngazi hiyo, mathalan katika shule za msingi imegawanyika katika namna kuu mbili; chini darasa la kwanza na pili, iko katika msingi wa kuelewa ‘KKK’ ikimaanisha Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.

Hatua hiyo mwanafunzi anaundwa na hata kuvushwa akamudu, maana ndio nyenzo ya kufahamu kuelewa, katika namna mbili; nadharia na hisabati.

Ngazi ya pili katika darasa la Tatu huwa ngazi ya mpito, ambayo alichokinasa kutoka KKK, sasa anaongezewa vya ziada taratibu anavyopaswa kujua katika tafsiri pana, huku ikiendelezwa KKK, kumkomaza.

Maboresho yanaendelea kwa hiyo ziada na kukuza KKK, kukionekana masomo kama; Historia, Jiografia na Uraia akiaminika anajua kutafakari kwa ngazi hiyo ya awali, akitambulishwa ya ziada.

Mwanafunzi ananolewa kuanzia vitendea kazi vya msingi KKK, huku akitanuliwa uelewa wake katika matumizi ya ziada ambayo tabia inayomuongezea mengi.

Kitabu kinampatia mwanafuzi ya ziada nje ta darasani, lakini yanayohusiana na anachopaswa kukijua kiwango chake. Hicho ni kitabu kilichomo kwenye mtaala cha kiada (cha lazima), pia vya ziada (vya hiari, ila muhimu).

Vilevile, kitabu hicho kinamjengea mwanafunzi utamaduni wa kujisomea, ambao sasa umedora sana, hata akahamia katika magazeti, mambo yanayomjengea uwezo na mbinu nyingi za kisomi.

Kurejea msingi wa usomaji, ngazi kama za KKK huanza tena kidato cha kwanza, mitaala ikitambulisha somo na wasifu wake kimatendo.

Kadri msingi huo unasonga kufika kidato cha pili, taaluma ya ngazi hiyo inatanuka zaidi kwa masomo yaleyale, huku wanapofika vidato vya tatu na nne inazama maradufu.

Mathalan, masomo ya lugha zikishamuunda mtumiaji kwa sarufi, humtanua mtumiaji maarifa na uwezo wa kutumia na kutafakari kupitia fasihi, inayoanza kidato cha tatu.

Mtaala wa zamani (1976) ulikuwa na somo tofauti na hisabati (Basic Mathematics), ambalo nalo hisabati  waliruhusiwa wenye msingi mzuri katika hisabati ya awali.

Vivyo hivyo, katika masomo ya utunzaji mahesabu (Book Keeping) mwanafunzi anatumika kidato cha tatu na nne, kile afanyacho mhasibu mwandamizi ofisini.

MSOMI ALIYEKAMILIKA 

Alivyo mwanafunzi aliyetimia kimasomo haishii viashiria vya kufaulu pekee, bali yu mweledi katika matumizi ya maarifa na upeo aliyomegwea darasani.

Hiyo inajumuisha mbinu sahihi ya kunasa ufafanuzi wowote anaopewa, kisha anautafsiri kulinganisha na mahitaji yake katika kuelewa.

Kwa mfano, anamsikia akizungumza kwa Kiingereza, anamfuatilia kuoanisha na uelewa wake.

Ndio maana walimu wote ngazi mbalimbali, shuleni hadi vyuoni, wengi wananawarithisha wanafunzi vigezo vyao vikuu vinne vya kiualimu, wavitumie katika harakati za kujiwezesha kuelewa.

Hapo kuna saikolojia husika falsafa ya kile anajifunza, namna ya kujumuika nayo kitaaluma (kama vile mijadala), kuweka mipango ya kufanikisha kusoma, usimamizi wake, kisha anajifanyia tathmini kuu ‘nimeelewa au sijaelewa na kama sijaelewa, kwanini?”

Hayo yakirejewa kinyume, ndio yanashikilia mtaala kila mahali duniani taaluma ya ‘Elimu.’ 

Ni bahati mbaya, staili ya usomaji tuisheni unavuka vipengele hivyo vyote na kumuondoa mwanafuzi katika kujenga uwezo ajitegemee, anabaki kuwezeshwa kwa kukariri cha mwisho, bila ya kuzijua ngazi za kufikia jibu kwa ufasaha.

Uzao wa hayo, ndio unaibua tukio linalowaibua wanafunzi wa ngazi wa chuo kikuu wanamuomba notsi mhadhiri au darasa la tuisheni, hata nguli hao wanaachwa na butwaa.

Lakini, haishii hapo, katika chuo kingine chenye hadhi ya kutoa digrii, wanafunzi wanafunzwa kwa kugaiwa muhtasari wa maelezo (notes summary), mhadhiri akiwaahidi wakisoma vizuri “mtihani utatoka humo humo.”

Ni kinyume na uhalisia wa hitaji la mwanachuo kushinikizwa asome vitabu na marejeo mbalimbali, kupanua uelewa wake hata akajua mengi, hukuhuko mbinu zake za kusoma zinaongezeka.

Staili hiyo inaonyesha kuwa mhadhiri au mkufunzi wa ngazi hiyo ama ni muumini au zao la tuisheni, akihamisha mbinu ya kusoma chuoni, kutoka mwanafunzi ya darasani, akisadiwa kutumia ziada ya vitabu na mijadala kitaaluma akaelewa.

KILICHOWEZEKANA ZAMANI

Katika moja ya shule ya sekondari zama hizo zikiwa chache kama zilivyo nyingine zilikuwa na shida ya walimu, hasa shule binafsi. 

Sehemu kubwa ya waliowafundisha   hawakuwana sifa sahihi, baadhi ni wahitimu wa kidato cha sita na kuna wakati baadhi ya masomo yalikosa walimu kwa wakati fulani. Muhtasari wa masomo (syllabus) uliotumika wakati huo ulikuwa wa mwaka 1976.

Kuna wanafunzi wakugundua hakuna mwalimu na mada hizo zinapita wakiwa kidato cha tatu kwa masomo ya Kemia na Fizikia, wakachukua muhtasari wa masomo, pia vitabu maarufu vya masomo.

Kwa Kemia ni kitabu cha Michael Neklon na Fizikia A.F Abott, wakazifanya marejeo kujisomea, kisha kuandaa notsi zao  kwa mafanikio, kana kwamba wamesoma tuisheni au darasani, hata wakamudu kujibu maswali ya mtihani iliyopita katika waliojifunza.

Walioprejea likizo majumbani, waliomba notsi za wenzao wakazinakiri, kisha kujifunza zaidi, maana wakati huo ilikuwa adimu kuwa na huduma tuisheni utoaji nakala ya maandishi.

Nini siri ya mafanikio hapo? Ni kwamba wasomaji hao walikuwa na mbinu ya kujitathmini mipango yao kuwanuia kufaulu na matundu yaliyoko mbele yao.

Pia, wakajiwekea mipango kitaaluma na wakajisimamia, kisha wakaitekeleza, kwa kuwa stali zote za kujisomea walikuwa nayo, ikiwamo kusoma vitabu.

Pia, inaendana na kupitia muhtasari wa kujifunza na kujua wanayopaswa kuyajua kwa masomo mbalimbali, hivyo ni wanafunzi wanaojua wanakotoka, waliko na waendako, wakijiwekea mkakati kuvuka daraja la mtihani kitaifa kuelekea ng’ambo ya pili. Ni ngumu kwa mwanafunzi mwenye wasifu huo, kwenda kuomba tuisheni chuoni.