Kampeni ya Samia Legal Aid yawafikia wananchi milioni mbili

By Allan Isack , Nipashe
Published at 02:17 PM Apr 01 2025
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi, akizungumza na raia wa kigeni katika Kata ya Malula wilayani Arumeru mkoani Arusha,wakati wa uzinduzi wa kiwilaya wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Samia Leagal Aid.
Picha: Allan Isack
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi, akizungumza na raia wa kigeni katika Kata ya Malula wilayani Arumeru mkoani Arusha,wakati wa uzinduzi wa kiwilaya wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Samia Leagal Aid.

Wizara ya Katiba na Sheria imesema kuwa kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Samia Legal Aid, wamefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya milioni mbili (2,000,000) kutoka mikoa mbalimbali nchini tangu ilipoanza mwaka 2023.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa wizara hiyo, Ester Msambazi, wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika ngazi ya wilaya, uliofanyika Kata ya Malula, wilayani Arumeru, mkoani Arusha.

Msambazi amesema kuwa kampeni hiyo inatekelezwa nchi nzima na hadi sasa wamefika mikoa 23, huku wakibakiza mikoa mitatu ili kukamilisha mpango huo.

"Tumeshakutana na wananchi zaidi ya milioni mbili moja kwa moja, na pia tunatumia vyombo vya habari kuwafikia watu wengi zaidi ya tunaokutana nao ana kwa ana," amesema Msambazi.

Ameeleza kuwa lengo kuu la kampeni ya Samia Legal Aid ni kuwasaidia wananchi wenye changamoto za kisheria, hususan wale wasioweza kumudu gharama za kuajiri mawakili wa kuwatetea mahakamani.

"Kwa upendo wake kwa wananchi, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alielekeza Wizara ya Katiba na Sheria kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa umma ili kuwajengea uelewa kuhusu taratibu za kisheria, haki zao, na wajibu wao," amesema Msambazi.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha,Amir Mkalipa, akizungumza wakati akifungua Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Samia Leagal Aid, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria Damas Ndumbaro,uzinduzi wa kampeni hiyo ulifanyika kiwilaya katika Kata ya Malula wilayani humo. PICHA: ALLAN ISACK

Ameongeza kuwa kampeni hiyo inalenga pia kuwapatia msaada wa kisheria wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za wanasheria, sambamba na kuwajengea wananchi uwezo wa kuelewa masuala muhimu ya kisheria.

"Tuko hapa kwa ajili ya kutoa mada mbalimbali zinazohusu sheria, pamoja na ushauri wa kisheria kwa wale wanaohitaji msaada huo," amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amir Mkalipa, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro, ameishukuru wizara kwa kuleta kampeni hiyo kwa wananchi wa wilaya yake.

Amesema kuwa kupitia kampeni hiyo, wananchi wanapata fursa ya kupata elimu ya kisheria itakayowasaidia kutambua njia sahihi za kutafuta haki zao.

"Hii ni siku muhimu sana kwa sababu inalenga kufanikisha upatikanaji wa haki kwa wananchi waliodhulumiwa lakini hawakujua namna ya kuitafuta. Kupitia kampeni hii, wataalamu wa sheria watawasikiliza na kuwasaidia kutatua changamoto zao," amesema Mkalipa.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi,akizungumza katika Kata ya Malula wilayani Arumeru mkoani Arusha, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Samia Leagal Aid.PICHA: ALLAN ISACK