Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa ana "hasira kubwa" na "amechukizwa" na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, baada ya wiki kadhaa za majaribio ya kusitisha mapigano nchini Ukraine.
Katika mahojiano na NBC News, rais huyo wa Marekani alisema anakerwa na Putin kwa kushambulia uhalali wa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, na alitishia kuweka ushuru wa hadi 50% kwa nchi zinazouza mafuta ya Russia ikiwa Putin hatakubali kusitisha mapigano.
"Ikiwa mimi na Urusi hatuwezi kufanikisha makubaliano ya kusitisha umwagaji damu Ukraine, na ikiwa nitahisi kuwa ni kosa la Urusi, ambalo huenda siyo... nitaweka ushuru wa ziada kwa mafuta yote yanayotoka Urusi," alisema Trump.
Kauli hizi zinaashiria mabadiliko katika msimamo wa Trump kuhusu Putin na Russia. *kulu ya Marekani haijatoa tamko rasmi kuhusu suala hili.\
Viongozi wa Ulaya walikuwa na wasiwasi kuwa Trump alikuwa karibu sana na Putin wakati mazungumzo ya kusitisha mapigano Ukraine yakiendelea.
Kwa wiki sita zilizopita, Trump amekuwa akimshinikiza Zelensky kwa masharti kadhaa huku akimfurahisha Putin na kukubaliana kwa kiasi kikubwa na matakwa yake.
Lakini hali inaonekana kubadilika. Hii ni mara ya kwanza kwa Marekani kutishia kuiwekea Vita Urusi vikwazo kwa kuchelewesha mazungumzo ya amani, jambo linaloipa Moscow mzigo wa kuchukua hatua.
Kwa mujibu wa NBC News katika mahojiano ya simu ya dakika 10, Trump alisema alikuwa na hasira kubwa wakati Putin alipomdharau na kudharau hadhi ya Zelensky, ingawa Trump mwenyewe hapo awali alikuwa amemwita Zelensky dikteta na kumshinikiza afanye uchaguzi.
"Unaweza kusema nilikuwa na hasira sana, nimechukizwa, wakati... Putin alipoanza kushambulia uaminifu wa Zelensky, kwa sababu hiyo siyo njia sahihi ya kwenda," alisema Trump.
"Uongozi mpya unamaanisha hutakuwa na makubaliano kwa muda mrefu," aliongeza. Trump alisema Warusi wanajua kuwa amekasirika, lakini akasisitiza kuwa ana "uhusiano mzuri sana" na Putin na kwamba "hasira hupungua haraka... ikiwa atafanya jambo sahihi."
Iwapo Urusi haitakubali kusitisha mapigano, Trump alitishia kuiwekea vikwazo zaidi vya kiuchumi ikiwa atahisi kuwa ni kosa la Putin.
Chanzo: BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED