Wasira amjibu Zitto kuhusu vikao vya CHADEMA

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:52 PM Mar 31 2025
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira.
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amemjibu Kiongozi Mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kuhusu masuala ya vikao vya chama cha CHADEMA, akisema kuwa CCM haibishani na CHADEMA kwa sababu walishawambia wajiandike na kutoa majibu yao badala ya kupoteza muda.

Wasira alitoa majibu hayo wakati akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Machi 30, 2025, akieleza kuwa CCM haijakataa vikao na CHADEMA. 

Alisema kuwa wakati wa Zitto Kabwe aliposema kuwa CCM haiko tayari kujibu masuala yao, CCM walijibu kuwa wanataka majibu kutoka kwao na kwamba kama hawako tayari kutoa majibu, waambie Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

“Nilisema tuzungumze, Tundu Lissu akasema tutawapotezea muda, sasa mtu ana muda wake na hataki kupoteza muda wake, kwa hiyo sisi tunawaambia wakiwa na jambo linazungumzika waje tuzungumze,” alisema Wasira.

Alisema kwamba CHADEMA hawajatoa majibu wazi kuhusu mabadiliko wanayoyataka, na kwamba wanachama wa chama hicho sasa wameanza kuwageuka. Aliwasihi waeleze bayana ni mabadiliko gani wanayohitaji na kama wanashindwa, basi waambie Watanzania kile wanachotaka.

1

Wasira alizungumzia pia madai ya Zitto Kabwe kwamba CCM imekataa kukaa na CHADEMA, akisema kuwa ni jambo lisilo la kweli. Alifafanua kuwa CCM ni mwanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ambacho mwenyekiti wake ni Tundu Lissu, na kwamba kama Lissu ataita kikao, CCM itahudhuria kwa kuwa wao ni watu wa amani na hawataki migogoro.

“Wakati akiwa Lindi, Zitto alijua historia ya CCM. Hivyo basi, wanatakiwa kueleza ni mabadiliko gani wanayotaka,” alisema Wasira.
2