TIMU ya Mtibwa Sugar sasa inahitaji pointi 11 tu kuweza kurejea tena kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuteremka msimu uliopita.
Ushindi wa mabao 3-1 uliuipata juzi kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro dhidi ya TMA, umeifanya timu hiyo kufikisha pointi 60, ikihitaji pointi 11 ifikishe pointi 71 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu yoyote ile.
Mtibwa, ambao ni vinara wa Ligi ya Champioship kwa muda mrefu, imesalia na michezo mitano kabla ya kuhitimisha michezo yake msimu huu.
Kwa maana hiyo inahitaji ishinde angalau michezo minne ili kujikusanyia pointi 12, katika michezo iliyobaki ili ipate nafasi ya kupanda moja kwa moja Ligi Kuu bila kusubiri mechi za mchujo.
Kimahesabu, Mtibwa itakuwa imepanda kwani timu zinazoifuatia, Mbeya City na Stand United ambazo zote zina pointi 52, kama zikishinda michezo yao yote sita itakayobaki zitafikisha pointi 70 tu.
Kwenye uwanja wa Manungu Complex, mashabiki wa timu hiyo walikuwa wameshika vipeperushi ambavyo vilikuwa na ujumbe au kauli mbiu isemayo, 'ukishuka ujue kupanda', ambavyo viliongeza chachu kwa wachezaji wa timu hiyo na burudani uwanjani.
Mtibwa, ilishuka daraja mwishoni mwa msimu uliopita, lakini imeonekana kupigana kufa na kupona kuhakikisha inarejea tena Ligi Kuu.
Fredrick Magata, ndiye aliyeanza kuona nyavu za TMA mapema tu dakika ya tatu, kabla ya yeye mwenyewe kuweka kamba nyingine dakika ya 15 ya mchezo. Bao la tatu lilifungwa na Omari Marungu katika dakika ya 32.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Magata, alisema anashukuru kuifungia timu yake mabao mawili akiweka wazi lengo ni kurejea Ligi Kuu huku akiwataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwapa sapoti kwenye michezo iliyobaki.
"Tumefika pazuri, lakini mechi zilizobaki pia ni ngumu kwa sababu ni za maamuzi, tunaomba mashabiki waendelee kutusapoti kama hivi wanavyofanya ili tufikie malengo tuliyojikwekea," alisema mchezaji huyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED