Mrema asikitika shambulio kiongozi BAWACHA,ashangaa msimamo wa chama

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:16 PM Mar 31 2025
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema.
Picha: Mtandao
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, ameonesha masikitiko yake kuhusu taarifa iliyotolewa na chama hicho kuhusiana na tukio la shambulio dhidi ya kiongozi wa wanawake taifa wa chama hicho (BAWACHA).

Mrema alieleza kushangazwa na msimamo wa chama kuhusu tukio hilo, akieleza sababu kadhaa zilizomfanya kutoridhishwa na taarifa hiyo.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter), Mrema alikosoa chama cha CHADEMA kwa kutoona umuhimu wa kulaani kitendo cha kiongozi wa wanawake kupigwa na kuumizwa na mwanaume, huku chama kikidai kuwa ni taarifa inayosambazwa mitandaoni. 

Alisema kuwa hatua hii inaonyesha kutokuwepo kwa mshikamano wa ndani ya chama na kutojali hali ya mwanachama aliyeathirika.

“Chama kilishindwa kutoa pole kwa kiongozi huyo, licha ya kuwa mara nyingi kimekuwa kikitoa pole kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanapopatwa na majanga,” alisema Mrema.

 Alieleza kuwa kutotoa pole kwa kiongozi huyo kunaleta maswali kuhusu utamaduni wa chama katika kushughulikia masuala ya ndani, hasa yale yanayohusiana na ustawi wa wanachama wake.

Mrema pia alikosoa kauli ya chama inayosema kinachunguza tukio hilo, lakini kwa upande mwingine kikitoa vitisho kwa mhanga wa shambulio hilo. 

Alisema kuwa hatua hiyo inazua taharuki na inaweza kuathiri upatikanaji wa ukweli kuhusu tukio husika.

Zaidi ya hayo, Mrema alilalamikia kauli za chama ambazo alizilinganisha na zile zilizokuwa zikitolewa wakati wa uongozi wa Hayati John Magufuli, akihusisha na matukio ya watu kupotea na ukandamizaji wa haki za binadamu.

Katika tamko lake, Mrema amesisitiza kuwa analaani vikali kitendo cha kiongozi wa wanawake kupigwa na wanaume, akikitaja kuwa ni ukatili wa kijinsia unaopaswa kupingwa na kila mtu mstaarabu bila kujali ni nani aliyekumbwa na tukio hilo.

Ameongeza kusema kuwa ukatili huu hauna tofauti na vitendo vingine vya kikatili vinavyowakumba wanawake nchini, na hivyo akatoa wito wa mshikamano wa pamoja katika kupinga matendo kama haya, ndani na nje ya vyama vya siasa.