Kocha Yanga aichimba mkwara Tabora United

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:29 PM Mar 31 2025
Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi, ni kama ameicbhimba mkwara klabu ya Tabora United kwa kuweka wazi kuwa ni lazima wawafunge kwenye uwanja wao wa nyumbani hapo kesho.

Kocha huyo amesema kuwa macho ya wanachama na mashabiki wote wa Yanga yapo kwa wachezaji ili kuona watafanya nini ili kulipa kisasi cha kufungwa mabao 3-1 kwenye mchezo wa kwanza, uliochezwa, Novemba 7 mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Amesema wachezaji wa Yanga wanalielewa hilo na wamewapa kazi ya kufanya ili kuwafanya wanachama na mashabiki kuwa na furaha baada ya maumivu waliyoyapata kwenye mchezo wa kwanza kwa kufungwa na Tabora United.

"Tunajua Tabora United ni timu bora, lakini lazima tukapambane," alimalizia kocha huyo.

Kocha huyo alizungumza hayo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la FA, ambapo timu yake ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Songea United na kuingia robo fainali.

"Nimefurahi tumeshinda na wachezaji hawakufanya makosa binafsi, nimefurahi kwa mara nyingine tena kuona wachezaji wangu ambao hawakuwa wanapata nafasi ya kucheza wamepata dakika nyingi za kufanya hivyo na wamefanya vizuri.

Nampongeza sana golikipa wa Songea United, amefanya kazi kubwa sana, ametupunguzia mabao mengi kwenye mchezo huu," alisema Miloud.

Kocha huyo alikuwa akizumgumzia kipa wa Songea United, Khatib Mbwana, aliyekonga nyoyo za mashabiki wa soka kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam juzi kwa kuokoa michomo mingi ya hatari kutoka kwa wachezaji wa Yanga na kupunguza idadi ya mabao ambayo ingeweza kukutana nayo.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Songea United, Meja mstaafu, Abdul Mingange, alisema waliingia kwenye mchezo huo kwa kuiheshimu Yanga, lakini bila kuwapa presha wachezaji wao ya kuwalazimisha kushinda mechi hiyo.

 "Yanga ni timu kubwa, ndiyo maana niliwaambia wachezaji wangu wakae nyuma, niliwaambia wakipata mpira wasiutupe, vinginevyo wataadhibiwa,  hatukuwapa presha vijana wetu kuwa lazima tushinde leo, hapana.

Lengo langu lilikuwa tucheze mpira mzuri, hata kama tutafungwa lakini mashabiki wavutiwe na soka tutakalocheza," alisema Meja Mingane.

naye pia alimsifia kipa wake Mbwana, ambaye alifanya kazi kubwa, akisema walimtoa kwenye kikosi cha vijana cha Coastal Union.