Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewakumbusha Wananchi kuyatenda mambo yote mema walioyatekeleza wakati wa Ramadhani ikiwemo Ibada pamoja na kuiombea Nchi Amani ikielekea Uchaguzi Mkuu Mwezi Oktoba Mwaka huu.
Rais Dk. Mwinyi amesema hayo alipozungumza katika Baraza la Idi liliofanyika Ukumbi wa Chuo cha Polisi Ziwani, Wilaya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 31 Machi 2025.
Aidha amezihimiza mamlaka zinazosimamia sheria za usalama barabarani kuzisimamia ipasavyo Ili Kuepusha ajali zinazoweza kuepukika katika kipindi cha Sikukuu ya Idd El Fitri.
Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa wakati wa sikukuu harakati za Usafiri wa Vyombo vya moto huongezeka Barabarani hivyo Mamlaka zina Wajibu wa kuhakikisha Usalama wa Watumiaji wa Barabara kwa kusimamia Sheria kikamilifu.
Amefahamisha kuwa ni vyema Usalama wa Watoto ukaimarishwa katika Viwanja vya Sikukuu ili Wananchi Washerehekee Sikukuu kwa Furaha na Amani kwa kudhibiti viashiria vyote vya udhalilishaji na uvunjifu wa Amani.
Halikadhalika Rais Dk. Mwinyi amewahimiza Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi kwa ujumla kuendeleza Mwenendo wa kuwasaidia Watu wenye Mahitaji mbalimbali wakiwemo Watu wenye Ulemavu, Wajane,Wazee,Yatima na Watu Wanaoishi katika Mazingira Magumu kwa Kuwapa Sadaka kwa kiwango kilichooneshwa wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kwa upande mwingine Rais Dk. Mwinyi amewashukuru Waumini Wasio Waislamu kwa Kutoa Ushirikiano wa kutosha kwa Waislamu wakati wa Mwezi wa Ramadhani kuwa ni kielelezo cha Ustahamilivu kwa Waumini wa Madhehebu tofauti Jambo alilolisisitiza kudumishwa kwa Manufaa ya nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED