Wananchi wametahadharishwa kuwa makini katika kuchagua viongozi wanaowafaa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa kuhakikisha wanawachagua viongozi wanaojali matatizo yao badala ya wale wanaotoa “vijisent,” ambao wanaweza kuwa mzigo kwao kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Tahadhari hiyo imetolewa leo Machi 31, 2025, na Sheikh wa Wilaya ya Shinyanga, Soud Kategile, wakati wa hotuba yake mara baada ya swala ya Eid iliyoswaliwa katika mkoa huo, ikiongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya.
Sheikh Kategile amesisitiza kuwa mwaka huu Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge, na rais, hivyo ni muhimu kwa wananchi kuwa waangalifu na kufanya maamuzi sahihi kwa kuwachagua viongozi wenye sifa bora, wanaopenda maendeleo na wanaojali matatizo ya wananchi.
"Uchaguzi mkuu wa mwaka huu, mchague viongozi wanaowafaa na siyo watoa 'vijisent,' kwani itawagharimu ndani ya miaka mitano ijayo," amesema Sheikh Kategile.
Aidha, amewasihi waumini wa dini ya Kiislamu kuendeleza matendo mema hata baada ya mfungo wa Ramadhani kumalizika, kwa kufuata mafundisho ya Mwenyezi Mungu kama walivyokuwa wakifanya katika kipindi cha mfungo.
Baadhi ya waumini walioshiriki swala hiyo pia wamewasihi wenzao kusherehekea Sikukuu ya Eid kwa utulivu na kushiriki na familia zao badala ya kujihusisha na anasa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED