Serikali yakusudia kuboresha mazingira ya kujifunzia

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 02:07 PM Mar 29 2025
Serikali imekusudia kuboresha mazingira ya kujifunzia katika shule nchini
PICHA: MTANDAO
Serikali imekusudia kuboresha mazingira ya kujifunzia katika shule nchini

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekusudia kuhakikisha mazingira ya utoaji wa elimu yanakuwa salama ili kuwasaidia walimu na wanafunzi kufikia malengo wanayokusudia hasa kupatikana kwa elimu bora.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk. Wilson Mahera alisema hayo mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo kwa walimu wanasihi 5,000 kutoka shule za msingi 5,000 zilizoteuliwa kutekeleza Afua ya Mpango wa Shule Salama kupitia Program ya BOOST kutoka halmashauri zote za wilaya na mikoa yote hapa nchini.

Akasema kwa sasa utoaji wa elimu katika shule za awali na msingi unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu isiyo rafiki na isiyotosheleza, mmomonyoko wa maadili katika jamii, kukosekana kwa huduma ya chakula, utoro wa walimu na wanafunzi, malalamiko mbalimbali ya wadau wa elimu na mazingira yasiyoridhisha ya utoaji wa elimu katika baadhi ya shule hali inayoathiri utoaji na upatikanaji wa elimu bora. 

"Ndiyo maana mafunzo haya yanalenga kuhakikisha changamoto zilizobainishwa zinakabiliwa ili kuwezesha mazingira mazuri ya ufundishaji na ujifunzaji, mafunzo yanalenga kusaidia kuimarisha utoaji wa huduma za ushauri na unasihi shuleni na jinsi ya kutatua na kushughulikia malalamiko mbalimbali ya walimu na wanafunzi" alisema Naibu Katibu mkuu huyo.

Naibu Katibu mkuu huyo alisema mafunzo hayo pia yanalenga kuimarisha stadi, maarifa na ujuzi wa walimu katika utekelezaji wa mpango wa shule salama katika shule sambamba na kusaidia kujua namna ya kubaini na kushughulika wanafunzi walio katika hatari ya kuacha shule na  kubaini na kushughulikia mapitio hatarishi kwa wanafunzi kutoka nyumbani kwenda shule na kurudi nyumbani.

Akaongeza kuwa mafunzo hayo yatakayofanyika katika vituo vitano ikiwemo vyuo vya Ualimu vya Morogoro ,Klerruu, Korogwe na Tabora yatasaidia kuboresha utendaji kazi na kuzingatia maadili katika kazi ya ualimu ,kuboresha na kuimarisha mahusiano kati ya shule na jamii ama wazazi kupitia ushirikiano wa wazazi na shule.

"Yatalenga pia kushughulikia na kutatua unyanyasaji wa kijinsia na kushirikiana na jamii kuhakikisha huduma ya chakula na lishe inatolewa shuleni, wapo baadhi ya wazazi wanachanganya mpango wa elimu bure na suala la kuchangia chakula kwa wanafunzi wakati jambo hili ni wajibu wao kama ambavyo wanaweza kuwapatia chakula watoto wawapo majumbani" alisisitiza Dk Mahera.

Naye Mkurugenzi wa Elimu Maalum kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia  Magreth Matonya alisema ni muhimu kwa watoto wenye mahitaji maalum kuhakikisha wanapata elimu stahiki ili waweze kufaulu katika elimu ya msingi na sekondari.

Akasema watoto wa aina hiyo wasipofaulu hugeuka mzigo kwa wazazi wao na jamii kwa ujumla hivyo ni muhimu  sana wakawa katika mazingira salama ili wasome vizuri na kufaulu masomo yao.