Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, amesema hataki kusikia tena kuhusu changamoto ya upatikanaji wa dawa katika Hospitali ya Utete na kumtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Hamis Abdallah, kuhakikisha anashughulikia tatizo hilo ili wananchi waendelee kupata huduma bora.
Mchengerwa ametoa maelekezo hayo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji katika Hospitali ya Wilaya ya Rufiji, iliyopo Utete.
"Mganga Mkuu, umepata nafasi ya kuja Rufiji, hivyo unapaswa kushirikiana na wasaidizi wako kutatua changamoto ya kutopatikana kwa dawa katika eneo hili, ambalo mimi ni Waziri wa TAMISEMI," Mchengerwa amesisitiza.
Waziri Mchengerwa ameeleza kuwa, Rufiji haijawahi kukutana na changamoto hiyo ya ukosefu wa dawa na kutolea mfano kipindi alichokuwepo Dk. Makenge, ambaye aliwahi kuwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rufiji.
"Mganga Mkuu, suala hili halifurahishi. Sitaki wananchi walalamike tena kuhusu kukosa dawa. Jipange kuhakikisha kuwa dawa hazipungui, na nitafanya uchunguzi ili kubaini tatizo ni nini, kwani Serikali haina tatizo la fedha za madawa," ameongeza Mchengerwa.
Aidha, Mchengerwa amewapongeza Waganga Wakuu na watumishi wa kada ya afya kwa juhudi zao katika kupunguza vifo vya mama na mtoto na kudhibiti vitendo vya rushwa, hususan dhidi ya akina mama wanaofuata huduma ya afya ya uzazi katika hospitali na vituo vya afya nchini.
Naye, Mmoja wa wananchi wa Wilaya ya Rufiji, Mwema Said, ametoa shukrani kwa Waziri Mchengerwa kwa kuboresha miundombinu katika Hospitali hiyo ambayo kwasasa wananchi kufurahiya wodi zilizojengwa, vifaa tiba vilivyonunuliwa, pamoja na huduma bora zinazotolewa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED