Opresheni linda Demokrasia yazinduliwa rasmi Lindi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:07 PM Mar 29 2025
Kiongozi wa Chama Mstaafu Zitto Kabwe
Picha: Mpigapicha Wetu
Kiongozi wa Chama Mstaafu Zitto Kabwe

Chama cha ACT Wazalendo kimezindua rasmi Oparesheni Linda Demokrasia katika Mkoa wa Lindi, ikiwa ni sehemu ya harakati za kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda demokrasia na kupigania mabadiliko mbalimbali ya uchaguzi.

Oparesheni hiyo inalenga kusambaa kote nchini ili kukutana na wanachama wa chama pamoja na Watanzania kwa ujumla, kwa lengo la kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kuwa na mifumo huru na yenye uwazi katika michakato ya uchaguzi.

Katika kongamano la uzinduzi wa oparesheni hiyo, Kiongozi wa Chama Mstaafu, Zitto Kabwe, alikuwa mgeni rasmi. Akiwa mkoani Lindi, Zitto alisisitiza umuhimu wa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na kueleza kwamba, licha ya kupitishwa kwa Sheria mpya ya Tume Huru ya Uchaguzi, bado kuna changamoto katika utekelezaji wake.

Zitto alieleza kuwa sheria hiyo ilipitishwa kwa kura nyingi za wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na baadaye kusainiwa na Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu.

Aidha, Zitto alibainisha kuwa kuna haja ya kufanyika kwa mabadiliko ya mifumo mbalimbali ya uchaguzi pamoja na mabadiliko madogo ya katiba, kwani bado kuna muda wa kuyafanikisha.

Katika hotuba yake, alihimiza wananchi kupigania demokrasia ili heshima ya kura ya wananchi irejee. Pia aliwataka wasikate tamaa, akieleza kuwa kupigania demokrasia kuna gharama, lakini ni muhimu kwa ustawi wa taifa.

Oparesheni Linda Demokrasia ni azimio la Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo, lililofikiwa baada ya tafakuri ya kina kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa.