SERIKALI imewaagiza wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache kuhakikisha rudisho la uwekezaji katika kampuni wanazoziongoza kuongezeka kutoka asilimia saba ya sasa hadi kuzidi asilimia 10 mwaka ujao wa fedha.
Agizo hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka wilayani Kibaha mkoani Pwani, wakati wa kufunga mkutano wa siku tatu wa wakurugenzi wa bodi za kampuni hizo.
“Niwape changamoto ya kukuza rudisho la uwekezaji kutoka asilimia saba ya sasa kwenda zaidi ya asilimia 10 kwa mwaka. Na ili kufikia azma hii mnapaswa kuongeza ufanisi wa utendaji," aliagiza.
Aidha, aliwaagiza kuongeza ufanisi na gawio kwa serikali akisema, “Ninaamini mwaka ujao wa fedha mtatoa gawio kutoka taasisi mnazosimamia likiongezeka. Hiyo ni changamoto ninayowaachia".
Alisema kwa mwaka wa fedha uliopita, serikali ilipata gawio la Sh.bilioni 195 kutoka kampuni zake ambazo ina umiliki wa hisa chache.
“Mafanikio yetu yataakisi juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambazo zimekuwa zikifanyika za kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya biashara,” alisema Dk. Kusiluka.
Pamoja na mambo mengine, Dk. Kusiluka alionesha imani yake kwa mwongozo ulioboreshwa wa wakurugenzi wa bodi wa hisa chache uliozinduliwa mwanzoni mwa wiki hii wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere.
“Nimeupitia kwa kina na nimeona uko vizuri na utaisaidia serikali kutekeleza majukumu kwa weledi na kwa wakati,” alisema Dk. Kusiluka, huku akiipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kutengeneza mwongozo huo.
Hivyo aliwaelekeza wakurugenzi wa bodi kuutumia kikamilifu mwongozo huo ili kuongeza ufanisi katika maeneo yao.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amewataka wawakilishi wa serikali kwenye bodi za kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Pia,aliwataka wawakilishi hao ambao ni wakurugenzi wa bodi kuzitendee haki nafasi walizopewa ili kuhakikisha kuwa serikali inanufaika na uwekezaji iliofanya kwenye kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache.
“Nyie ni jicho la serikali hivyo mnapaswa kutokuchukulia kiwepesi nafasi mlizopewa, vinginevyo mtakuwa hamuitendei haki serikali na watanzania wote kwa ujumla,” alisema Mchechu.
Aliongeza: “Lazima mjidhatiti na kama unaona hauko kwenye nafasi ya kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na muda wa kutosha, ni vyema ukasema ili nafasi hiyo wapewe wengine.”
Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia taasisi 308 ambapo kati ya hizo 56 ni zile ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.
Jumla ya uwekezaji wa Sh.trioni 86.3 umefanywa katika taasisi hizo, kati ya kiasi hicho Sh.trioni 2.9 zikiwekezwa kwenye kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache na Sh.trioni 83.4 kikienda kwa taasisi ambazo serikali ina umiliki wa asilimia 100.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED