Zaidi ya watu 1,000 wafariki katika tetemeko Myanmar

By Enock Charles , Nipashe
Published at 02:21 PM Mar 29 2025
Hali ilivyo baada ya tetemeko huko nchini Myanmar
PICHA: MTANDAO
Hali ilivyo baada ya tetemeko huko nchini Myanmar

Zaidi ya watu 1,000 wamekufa nchini Myanmar na wengine zaidi ya 2,000 kujeruhiwa kufuatia tetemeko kubwa la ardhi ambalo lilisikika pia katika nchi jirani ya Thailand.

Wako wafanyakazi zaidi ya 100 Thailand waliokuwa wanaendelea na shughuli za ujenzi wa ghorofa moja hawajapatikana baada ya jengo hilo kubomoka. Wengi ya walioaga dunia wako Mandalay, mji wa pili kwa ukubwa nchini Myanmar, na mji ulio karibu zaidi na kitovu cha tetemeko la ardhi.

Wafanyakazi wa uokoaji bado wanahangaika kutafuta manusura nchini Myanmar na Thailand "Tunafukua watu kwa kutumia mikono," timu moja ya uokoaji iliambia BBC huko Mandalay, sio mbali na kitovu cha tetemeko hilo.

Shughuli za uokoaji zinaendelea katika eneo la juu ambalo halijakamilika huko Bangkok baada ya kuporomoka na takriban wafanyakazi 100 wa ujenzi hawajulikani waliko na sita wamekufa, kulingana na maofisa wa serikali ya eneo hilo.

Serikali ya kijeshi ya Myanmar imetoa ombi la msaada wa kimataifa, ombi adimu kutoka kwa serikali iliyojitenga na ambayo. imewekewa vikwazo vikali na mataifa ya Magharibi katika miaka ya hivi karibuni.

Udhibiti mkali wa jeshi la Myanmar na kuendelea kukosekana kwa utulivu wa ndani kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo kunafanya kuwa vigumu kupata taarifa sahihi kuhusu maafa hayo.