Msajili wa Vyama: Tayari tumechukua hatua stahiki dhidi ya Makalla

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:05 AM Mar 26 2025
Msajili wa vyama vya Siasa Nchini Jaji Francis Mutungi.
Picha:Mtandao
Msajili wa vyama vya Siasa Nchini Jaji Francis Mutungi.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imejibu ombi la ACT Wazalendo kuhusu kuchukuliwa hatua dhidi ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, ikieleza kuwa tayari ilishachukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258, hata kabla ya kupokea malalamiko hayo.

Katika barua yake ya tarehe 25 Machi 2025, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alieleza kuwa ofisi yake hufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuchukua hatua bila kusubiri mapendekezo kutoka kwa mtu au taasisi yoyote.

"Msajili anakushukuru kwa mapendekezo yako na anapenda ufahamu kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa huchukua hatua kwa mujibu wa sheria, hata bila ya mapendekezo ya mtu au taasisi yoyote," imeeleza sehemu ya barua hiyo.

ACT Wazalendo, kupitia Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu, walikuwa wamewasilisha malalamiko dhidi ya Makalla wakitaka achukuliwe hatua kwa kauli alizotoa katika mkutano wa hadhara mkoani Simiyu tarehe 22 Machi 2025. Makalla alidai kuwa CHADEMA inaendesha harambee ya kununua virusi vya M-pox na Ebola kwa lengo la kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025, kauli ambazo ACT ilizitaja kuwa za kizembe na zenye lengo la kuzua taharuki.

Hata hivyo, Ofisi ya Msajili haikufafanua hatua mahsusi ilizochukua lakini imehakikishia kuwa inatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Barua ya msajili.