Rais Samia afuturisha watoto Kikombo Dodoma

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 02:08 PM Mar 26 2025
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis.

Rais Samia Suluhu Hassan amewafuturisha Watoto wanaolelewa katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Dodoma katika Kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Akizungumza wakati wa Iftari hiyo kwa niaba yake, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi yenye lengo la kuondoa kabisa changamoto zinazowakabili watoto walio katika mazingira hatarishi. 

“Kipekee kabisa, ninamshukuru tena Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kufuturisha watoto wanaoishi katika Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo pamoja na maeneo mengine ya nchi hususani Watoto wa Mkoa wa Arusha na Dar es Salaam,"ameeleza.


Aidha ameongeza kuwa Wizara inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na wadau kwa lengo la kuhakikisha watoto walio katika mazingira hatarishi wanapatiwa huduma ya malezi ya muda mfupi katika Makao ya Watoto.