MATUKIO ya uhalifu na ulaghai kwa kutumia laini za simu za mkononi yamepungua katika Mkoa wa Singida kutoka 141 hadi kufikia 21 ilipofika Desemba 2024.
Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kati, Mhandisi Asajile John, alisema hayo wakati akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Maryprisca Mahundi, ambaye alifanya ziara juzi mkoani hapa.
Alisema hadi kufikia Desemba 2024 kulikuwa na laini za simu 2,019,928 kwa Mkoa wa Singida ukilinganisha na idadi ya watu 2,800,058 kwa mujibu wa sensa ya 2022 hivyo laini za simu na idadi ya watu ni takribani asilimia 100.8.
"Mkoa wa Singida wananchi pamoja na uwepo wa laini nyingi za simu wamekuwa wakizitumia vizuri ambapo matukio ya uhalifu na ulaghai kupitia simu za mkononi yameendelea kupungua ambapo kati ya Machi hadi Juni 2024 kulikuwa na matukio 141, Julai hadi Oktoba 67 na Oktoba hadi Desemba kulikuwa na matukio 21," alisema.
John aliwataka wananchi kuendelea kutumia vizuri mawasiliano na kujikinga na matendo ya uhalifu pamoja na kuchukua hatua kwa vyombo vinavyohusika wanapoona masuala ya utapeli.
"Kupitia kampeni mbalimbali zinazoendelea ikiwepo SITAPELIKI imesaidia kuelimisha wananchi ili wajielekeze kwenye mawasiliano yenye maana," alisema.
John aliongeza kuwa mawasiliano ya simu na intaneti hadi Desemba 2024 kulikuwa na minara iliyosimikwa kwenye mkoa wa Singida 225 ambayo imetapakaa katika wilaya zote ambapo kuna mawasiliano ya 2G,3G,4G na 5G.
"Wananchi wa Mkoa wa Singida sasa wameingia katika anga la kidigitali na wameingia kwenye intaneti ya kasi na hivyo kuwarahisishia kuingia kwenye uchumi wa kidigitali ambao unawarahisishia kwenye shughuli wanazozifanya," alisema.
TCRA mwaka jana ilizindua kampeni ya elimu kwa umma ikiwa na lengo la kuwakumbusha na kuwaelimisha watumiaji wa huduma za mawasiliano na wananchi umuhimu wa kutumia huduma hiyo kwa umakini ili kuepuka wizi na ulaghai wa kimtandao.
Kampeni hiyo ya TCRA inaongozwa na jumbe mbalimbali za elimu kwa umma zinazosisitiza; usitume pesa kwa mtu usiyemfahamu; hakiki ujumbe na namba inayokutaka utume pesa kabla ya kufanya muamala.
Msisitizo mwingine unaotolewa kwa wananchi ni mawasiliano baina ya mteja wa huduma za mawasiliano ya simu na mtoa huduma wake ni kuptia namba 100 pekee, kuepuka maelekezo yanayotolewa kupitia namba binafsi kuhusiana na huduma za mawasiliano ya simu.
Mengini ni kuepuka kufungua 'link' za mtandaoni usizozifahamu, kutochapisha chochote kuhusu watu wengine bila ridhaa yao; zuia mtu yeyote anayetuma maoni ya kukusumbua, kukutishia au yasiyofaa kuhusu wewe; toa taarifa kwa Jeshi la Polisi iwapo utapata shambulio la mtandaoni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED