DCEA yamkamata 'Mama Dangote' kinara biashara ya mirungi

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 01:59 PM Mar 26 2025
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanya operesheni maalum wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanya operesheni maalum wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanikisha utekelezaji wa ekari 285.5 za mashamba ya mirungi wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, kupitia operesheni maalum iliyofanyika kwa siku saba.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa saba (7) katika operesheni hiyo, akiwemo kinara mkubwa wa biashara haramu ya mirungi nchini, Interindwa Zinywangwa Kirumbi, maarufu kwa jina la Mama Dangote.

"Mama Dangote ni mzalishaji na msambazaji mkubwa wa dawa za kulevya aina ya mirungi nchini. Kwa zaidi ya miaka 30, amekuwa akiongoza mitandao ya biashara haramu ya mirungi na kusimamia masoko ya dawa hiyo," amesema Kamishna Lyimo.

Ameongeza kuwa Mama Dangote amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu, na operesheni hiyo imefanikiwa kumkamata, hatua muhimu katika kupambana na biashara haramu ya mirungi ambayo imekuwa ikisababisha madhara makubwa kwa jamii.

DCEA imeendelea kutekeleza juhudi za kupambana na dawa za kulevya nchini, na operesheni hii ni sehemu ya mapambano ya kuzuia uzalishaji, usambazaji, na matumizi ya dawa za kulevya, hususan mirungi.