Mpango Mgeni rasmi uzinduzi Mwenge wa Uhuru Kitaifa

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 02:54 PM Mar 26 2025
Picha za maandalizi ya Mbio za Mwenge Waziri Kikwete akikagua uwanja.
Picha: Julieth Mkireri
Picha za maandalizi ya Mbio za Mwenge Waziri Kikwete akikagua uwanja.

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa unaotarajiwa kufanyika Aprili 2, 2025, katika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, baada ya kukagua maendeleo ya maboresho ya uwanja utakaotumika kwa hafla hiyo.

"Napenda kutoa taarifa kuwa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa utafanyika Aprili 2, 2025, katika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango," amesema Waziri Ridhiwani.

Baada ya uzinduzi huo, Makamu wa Rais atawakabidhi Mwenge wa Uhuru kwa vijana sita walioteuliwa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambao wataendesha mbio hizo kitaifa katika mikoa 31 na halmashauri 195.

Waziri Ridhiwani ameongeza kuwa Mwenge wa Uhuru utaendelea kuhamasisha uwajibikaji na kupinga maovu kama uzembe, rushwa, ufisadi, na matumizi mabaya ya rasilimali katika miradi ya maendeleo.

"Falsafa ya Mwenge wa Uhuru ni chimbuko la matukio muhimu ya kihistoria kama Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, pamoja na Azimio la Arusha la mwaka 1967. Hivyo, ni jukumu letu kama Watanzania kuhakikisha tunauenzi mwenge huu kama ulivyoasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961," amesema Waziri huyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema maandalizi yanaendelea kwa kasi ili kuhakikisha uzinduzi huo unafanyika kwa mafanikio makubwa.

Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani, mikoa jirani, na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo.