Wajasiriamali nchini wanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazowazuia kufanikisha malengo yao, zikiwemo ukosefu wa mitaji, ujuzi wa biashara, nidhamu ya biashara, kukosekana kwa taarifa sahihi kuhusu soko, na changamoto za ubora wa bidhaa.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa AVODA Group, Jun Shiomitsu, wakati akieleza mkakati wa kampuni yake kuwainua na kuwawezesha wajasiriamali kupitia ubia wao na Unleashed Africa Social Enterprises.
Shiomitsu amesema kuwa licha ya wajasiriamali wengi nchini kuwa na biashara zenye mwelekeo mzuri, wanashindwa kuzikuza kutokana na ukosefu wa mbinu za ukuzaji wa biashara na uelewa mdogo wa masoko.
"Biashara zina changamoto nyingi sana, ili kuzikuza lazima wajasiriamali wajifunze mbinu bora za kuhudumia wateja, kutangaza bidhaa kwa ubunifu, na kushirikiana na wafanyabiashara wengine," amesema Shiomitsu.
Kutokana na hali hiyo, AVODA Group imeanzisha programu ya AVODA BLUE TZ, itakayowapa wajasiriamali mafunzo ya kina kuhusu ujasiriamali kwa muda wa miezi minne, kuanzia Julai mwaka huu.
Shiomitsu amesema programu hiyo itazingatia misingi ya dini ya Kikristo, lakini itakuwa wazi kwa watu wa dini zote wenye nia ya kujifunza. Mafunzo hayo yataendeshwa kwa vitendo, ambapo washiriki watajifunza mbinu za biashara na kuzitekeleza moja kwa moja.
"Tunataka kuona kama kweli mafunzo yanamsaidia mfanyabiashara kuongeza kipato. Ikiwa bado hajafanikiwa, tutamwongoza zaidi wakati akiwa ndani ya mafunzo," amefafanua.
Wajasiriamali watakaofaulu mafunzo hayo watapata fursa ya kuendelea na kozi ya miezi 12, ambayo itawasaidia kufungua milango ya uwekezaji kimataifa.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Unleashed Africa Social Enterprises, Khalila Mbowe, amesema ushirikiano wao na AVODA Group unalenga kuwawezesha wajasiriamali nchini kufanikisha malengo yao na kuongeza ufanisi wa biashara zao.
Mbowe amesema AVODA Group imevutiwa kuwekeza Tanzania kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji, sera za kidiplomasia zinazoweka mazingira bora ya biashara, na uhusiano mzuri kati ya Japani na Tanzania.
Programu hiyo itawajumuisha wajasiriamali waliokwisha anzisha biashara na wanaofanya mauzo, ili kuwasaidia kutambua changamoto zao na kuzitatua.
Mchakato wa kusajili wajasiriamali hao utatangazwa kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, makanisa, na mameneja wa kampuni mbalimbali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED