Wafanyabiashara wengine watatu wa Kariakoo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia kufuatia kuporomoka kwa jengo lililokuwa katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo.
Washtakiwa hao ni Soster Nziku (55) mkazi wa Mbezi Beach, Aloyce Sangawe (59) mkazi wa Sinza, na Stephen Nziku (28) mkazi wa Mbezi Beach.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani leo Jumatano, Machi 26, 2025, na kusomewa mashtaka yao kabla ya kuunganishwa na wenzao watatu, wanaodaiwa kuwa ni wamiliki wa jengo lililoporomoka.
Itakumbukwa kuwa Novemba 29, 2024, watu wanaodaiwa kuwa wamiliki wa jengo hilo, ambao ni Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61) mkazi wa Kariakoo, na Ashour Awadh Ashour (38) mkazi wa Ilala, walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka sawa na hayo.
Kwa sasa, washtakiwa wote sita wanakabiliwa na kesi hiyo huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini wahusika wengine wanaohusishwa na ajali hiyo mbaya iliyosababisha vifo vya watu 31.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED