Wadau wataja michepuko chanzo cha migogoro ya ndoa
By
Sabato Kasika
,
Nipashe
Published at 10:48 AM Mar 26 2025
Picha: Sabato Kasika
Prisica Ngweshemi akitoa somo.
Michepuko na wazazi kuingilia ndoa za watoto wao vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu za migogoro ya ndoa, hali inayosababisha ndoa nyingi kuvunjika au kuishiwa na maelewano.
Haya yameelezwa na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya makuzi, malezi, sheria, mazingira na afya yaliyofanyika Kisemvule, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani jana.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na shirika la Himiza Development Organization (HIDO) kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) yaliwahusisha wanawake kutoka kata mbalimbali za wilaya hiyo.
Pili Mkumbi, mmoja wa washiriki, alisema michepuko imekuwa kikwazo kikubwa katika ndoa, kwani wanaume wengi wamekuwa wakitoka nje ya ndoa na kusababisha familia zao kuingia kwenye hali ngumu ya maisha.
"Baadhi ya wanaume huacha kutoa matumizi katika familia zao baada ya kupata michepuko. Katika mazingira hayo, ni rahisi kusababisha migogoro. Hivyo, nyie mnaojua sheria, mtusaidie kujua namna ya kukabiliana na hali hii," alisema Pili.
Naye Biasha Ramadan alieleza kuwa baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiingilia ndoa za watoto wao kwa kuwapangia wake wa kuoa, jambo ambalo mara nyingi husababisha migogoro katika ndoa hizo.
Nancy Masenha akiendesha mafunzo."Unakuta kijana ameamua kumuoa mke anayempenda, lakini wazazi wanaingilia kati na kumshinikiza kuoa mwanamke kutoka kijijini kwao. Kitendo hiki kinaharibu ndoa," alisema Biasha.
Aliongeza kuwa amewahi kukumbana na hali hiyo, lakini alijitahidi kuvumilia hadi hali ilipotulia, na sasa anaendelea kuishi na mume wake baada ya kushinda vikwazo vilivyotishia ndoa yao.
Kwa upande wake, Mwanasheria kutoka LHRC, Nancy Msenha, alisema kuwa kituo hicho kimeweka milango wazi kwa watu wote wanaohitaji msaada wa kisheria ili waweze kupata suluhisho la migogoro yao, ikiwemo migogoro ya ndoa.
Naye Mkurugenzi wa Himiza Development Organization (HIDO), Prisca Ngweshemi, alisema kuwa kwa sasa jamii inakabiliwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili unaosababishwa na mambo mengi yanayofanyika bila uangalizi wa kutosha.
"Hata dhana ya 'mtoto wa mwenzio ni wako' imepotea. Ukimuona mtoto anafanya vitendo vibaya na ukajaribu kumkanya, wazazi wake wanakuja juu. Hali hii imewafanya watu kukata tamaa na kuacha mambo yaende ovyo," alisema Prisca.
Alisema kuwa vitendo hivyo vimechangia kuzorotesha malezi katika jamii, na mafunzo hayo yanalenga kusaidia kurejesha maadili mema kwa kufuata misingi sahihi ya makuzi na malezi.