Walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, wametakiwa kuanzisha miradi mbadala itakayowaingizia kipato ili waweze kujiimarisha kiuchumi.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, ameyabainisha haya leo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Kahama na kusema, serikali itawaunga mkono watakaonyesha jitihada za kuanzisha miradi hiyo.
Amesema, kila mwalimu anawajibu wa kutumia maeneo yanayomzunguka katika kuwekeza miradi mbadala ili kujiinua kiuchumi, kwani unapokuwa na kipato kizuri huwezi kushawishika kuingia kwenye mikopo inayosababisha wengi kuzimbia familia zao na wanafunzi kukosa masomo.
Mmoja wa walimu wa chama hicho, Revocatus Renatus, amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa kuliona hilo na kulisisitiza, kwani wengi wao wanaotegemea mshahara wameshindwa kujikwamua kiuchumi na kuingia kwenye mikopo umiza mitaani.
Nae mwalimu Stella Silayo amesema, uanzishwaji wa miradi hiyo itawasaidia kuepukana na changamoto mbalimbali za kimaisha, na watatumia maeneo yanayowazunguka katika uwekezaji ili wapate vipato mbadala.
Pamoja na ajenda mbalimbali zilizojadiliwa katika mkutano huo, pia ulilenga kufanyika uchaguzi utakaowapata viongozi wapya watakaokiongoza Chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Katibu wa Chama cha CWT mkoa wa Shinyanga, Kizito Shuli, amemtangaza Mwalimu Edina Kilambo kuwa Mwenyekiti wa CWT Kahama kwa kupata kura 95 dhidi ya mpinzani wake Vedastus Lugangila aliyepata kura 68.
Amewataka kushirikiana kwa pamoja na kuondoa makundi waliyokuwa nayo wakati wakiwakura ili kufikisha chama katika lengo lililokusudiwa hasa la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wanachama wao, ikiwemo wa kuepuka mikopo umiza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED