Baba ashikiliwa tuhuma za kuishi kinyumba na mtoto wake

By Christina Haule , Nipashe
Published at 06:57 PM Sep 09 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia Stanley Kunambi (45), mkazi wa Kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro, kwa tuhuma za kuishi kinyumba na binti yake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 13, na kufanya naye vitendo vya ngono kinyume cha sheria, ikiwemo kumbaka na kumuingilia kinyume na maumbile.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema tukio hilo liliripotiwa Septemba 1 mwaka huu, baada ya majirani kubaini viashiria vya mahusiano yasiyo ya kawaida kati ya baba huyo na mtoto wake.

“Mtoto huyu ni mwanafunzi wa darasa la saba. Tangu taarifa kuripotiwa, tumemkamata mtuhumiwa na tunaendelea na upelelezi, ikiwemo kumtafuta mama mzazi wa mtoto, ambaye anadaiwa kutengana na mtuhumiwa na kuwaacha watoto wawili chini ya malezi yake,” alisema Kamanda Mkama.

Baadhi ya majirani walisema walipatwa na mshangao mkubwa kufuatia tukio hilo, wakimtaka mtuhumiwa achukuliwe hatua kali za kisheria.

“Tulianza kuona dalili za ajabu, mfano mtoto kuishi chumba kimoja na baba yake, jambo lililotufanya tuhoji. Baada ya kufuatilia ndipo tukabaini ukweli,” alisema mmoja wa majirani.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kambitano, Kata ya Lukobe, Eliamini Kimaro, alithibitisha kupokea malalamiko hayo na kushirikiana na wananchi kufikisha taarifa Polisi.

Kwa sasa, mtoto huyo yupo chini ya uangalizi maalum wa Jeshi la Polisi na maofisa ustawi wa jamii ili kuhakikisha anapata msaada wa kisaikolojia na matibabu ya kiafya.