Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vyandarua kwa wananchi wa mkoa huo, huku akiwataka kuvutumia kwa malengo yaliyokusudiwa ya kujikinga na malaria.
Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika ofisini kwake leo Septemba 9, Kunenge amewataka wananchi kuacha kutumia vyandarua hivyo kwa shughuli zisizokusudiwa, ikiwemo kufugia vifaranga vya kuku na kuvulia samaki.
“Tunatakiwa kuhakikisha tunaondoa malaria kwa kuweka mazingira safi na kutumia vyandarua ipasavyo. Tusitumie vyandarua hivi kinyume cha utaratibu, maana madhara ya malaria ni makubwa kiafya na kiuchumi, hasa kwa watoto,” amesema Kunenge.
Ameongeza kuwa vyandarua vilivyogawiwa havina madhara yoyote, kwani vimepitia taratibu zote za kitaalamu, hivyo wananchi hawapaswi kusikiliza taarifa za upotoshaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji kutoka Bohari ya Dawa (MSD), Victor Sungusia, amesema ugawaji huo ni sehemu ya mpango mkakati wa Serikali wa kupambana na malaria. Alifafanua kuwa mkoa wa Pwani ni mkoa wa tatu kunufaika na mpango huo, baada ya Shinyanga na Kigoma.
“Mpaka sasa zaidi ya vyandarua milioni 40 vimeshagawiwa nchi nzima. Kwa mkoa wa Pwani pekee, vyandarua 1,200,000 vitagawiwa katika kaya zilizoainishwa ndani ya siku 21,” amesema Sungusia.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Kusirye Ukio, amesema kaya 454,595 zenye jumla ya watu 2,228,485 tayari zimetambuliwa na kutembelewa, sawa na asilimia 110 ya lengo, kwa ajili ya utaratibu wa ugawaji wa vyandarua hivyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED