Darasa la Saba kufanya mtihani kesho

By Restuta James , Nipashe
Published at 02:17 PM Sep 09 2025
Darasa la Saba kufanya  mtihani kesho
Picha: Mtandao
Darasa la Saba kufanya mtihani kesho

Wanafunzi 1,172,279 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, uliopangwa kufanyika kesho na kesho kutwa nchini, wakiwamo wavulana 535,138 na wasichana 637,141.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Septemba 9, 2025, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Profesa Said Ally Mohamed, amesema watahiniwa hao wanatoka shule 19,441 Tanzania Bara.

“Watahiniwa 1,094,321 sawa na asilimia 93.35 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 77,958 sawa na asilimia 6.65 watafanya kwa lugha ya Kiingereza,” amesema.

Amesema watahiniwa 4,699 wenye mahitaji maalumu watakaofanya mtihani huo wakiwamo wasioona, wenye uoni hafifu, uziwi, ulemavu wa akili na wa viungo.

Amesema watahiniwa watafanya mtihani wa masomo sita ambayo ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi pamoja na Uraia na Maadili.