Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema sifa alizonazo Mgombea Urais wa chama hicho, Dk. Samia Suluhu Hassan, zinatosha kumpa nafasi ya kuendelea kuongoza taifa kwa awamu nyingine ya mwaka 2025/2030.
Akizungumza Septemba 9, 2025, katika mkutano wa kampeni za urais uliofanyika katika Uwanja wa Bombadia, Dk. Bashiru alimuelezea Rais Samia kama kiongozi mwenye utulivu, ujasiri na umakini wa aina yake.
“Huyu kiongozi wetu ana utulivu wa pekee, ana ujasiri na umakini mkubwa. Sifa hizo ndizo zilizotuvusha katika kipindi kigumu cha janga la Covid-19 na kifo cha Rais Dk. John Magufuli. Matukio kama haya mara nyingi huacha maafa makubwa na kusambaratisha mataifa, lakini sisi tulibaki imara na taifa letu likabaki salama na moja,” amesema Dk. Bashiru.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya sifa binafsi za Rais Samia, lakini pia mchango wa CCM katika kuandaa na kulea viongozi.
“Kwa hiyo huyu si mgombea bora wa urais tu, bali ni mgombea bora wa urais wa chama bora. Tembea kifua mbele, utakumbukwa kama mwanamke aliyefanya mabadiliko makubwa katika nchi yetu,” ameongeza.
Aidha, amesema katika uongozi wa Rais Samia, kwa kuangalia sera, uamuzi na utekelezaji wa miradi mbalimbali, kumekuwa na mabadiliko makubwa hasa katika kuinua hali za wanawake nchini.
Kwa upande wake, Dk. Samia amewahakikishia wananchi kuwa uwekezaji unaofanywa na serikali yake nchi nzima ni kwa lengo la kujali utu wa kila Mtanzania.
“CCM imeweka ilani na kuelekeza uwekezaji mkubwa ili kuinua utu wa Mtanzania. Tunataka kila mmoja apate huduma bora za afya, elimu, usalama na ustawi wa kiuchumi. Kila tunachokifanya ni kwa ajili ya kujali utu wa Mtanzania,” amesisitiza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED