DARASA LA KABUDI KAMPENI ZA RAIS SAMIA; Aeleza historia mandhari Mbeya ilivyowakuna Wajerumani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:48 PM Sep 09 2025
Mwalimu Julius Nyerere (wa kwanza kulia), akipewa maelezo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa  Mbeya, John Mwakangale, walipotembelea kisima cha joto ardhi kilichoko  Kyejo wilayani Rungwe mwaka 1980. Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Kingunge Ngombare-Mwiru
Picha: JOHN MWAKANGALE MAKTABA
Mwalimu Julius Nyerere (wa kwanza kulia), akipewa maelezo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, John Mwakangale, walipotembelea kisima cha joto ardhi kilichoko Kyejo wilayani Rungwe mwaka 1980. Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Kingunge Ngombare-Mwiru

KWENYE kampeni za siasa ni darasa linalofungua mafaili ya mambo mengi kama uchumi, teknolojia, nishati maombi ya wapigakura na kwa ujumla msururu wa mafanikio, lakini ni nadra kusikia somo la historia likifundishwa.

Safari hii Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi, amewapa shule wananchi kuhusu historia ya Mbeya akiunganisha jinsi Wajerumani walivyougundua mkoa huo kuwa una uzuri wa asili na mandhari ya kipekee.

Anayasema hayo akizungumza katika kampeni za mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Samia Suluhu Hassan, Rungwe mkoani Mbeya, wiki iliyopita.

Waziri anataja mambo kadhaa yaliyowavuta Wajerumani mkoani humo ambayo sasa serikali imeyaibua na kuiinua Mbeya kwenye utalii, kitaifa na kimataifa.

Anakumbusha kuwa Filam ya Royal Tour inayoongozwa  na Rais Samia, imeipisha Mbeya zaidi kiutamaduni, kiutalii na kimafanikio ambayo serikali inakwenda kuwekeza.

Akichambua historia ya mkoa huo, anasema una utalii  wa mandhari ambao unaanzia enzi za Wajerumani ambao walipofika Mbeya walikumbuka walikotoka (nyumbani kwao) wakauita mji wa Mbeya ‘Langenburg’ sawa na jiji lililoko Ujerumani.

Aidha, anasema Tukuyu nayo ikaitwa ‘Noye Langenburg’ na kwamba kijiji cha Mano yaliko makao makuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) pia kipo Ujerumani na pia kinapatikana Poland.

Anaongeza kuwa walikiita kijiji hicho jina hilo kwa kukumbuka uzuri wa kule walipotoka.

Anakumbusha kuwa eneo la Ziwa Nyasa nalo Wajerumani wakaliita ‘Vida Hafen’ na kwamba yote hayo yanazungumzia uzuri wa mandhari ya mkoa huo yakilinganishwa na kile walichokiacha na wanachokikumbuka huko nyumbani kwao.

Anafafanua kuwa Mbeya ni bora kiutalii hasa wa mandhari ambao uliwavuta Wajerumani tangu awali baada ya kugundua uzuri wake.

Anasema awamu ya sita ya Rais Samia imeufungua utalii mkubwa wa mandhari na wengi hutembelea Tukuyu na kwa ujumla mkoa huo kuona uzuri usiomithilika wa eneo hilo 

Anasisitiza kuwa kupitia Filam ya Royal Tour, Mbeya na Rungwe zimefunguka akitoa mfano wa Hifadhi ya Bustani ya Maua ya Kitulo, ambayo inajulikana kwa wenyeji kama bustani ya Mungu.

“Hifadhi ya Kitulo ndiyo pekee duniani yenye maua na vipepeo kwa asili. Inaitwa Bustani ya Mungu. Rais Samia ameuonesha utalii huo duniani...”

“Nina hakika milima yote ya Rungwe na Livingstone mpaka Makete itaongoza kwenye utalii wa mandhari na afya. Watu watafika Mbeya kuona na kufurahia maajabu ya Mwenyezi Mungu katika mkoa huu,”

KASI MAENDELEO VIJIJINI

Akizungumzia mafanikio ya serikali ya Rais Samia Profesa Kabudi, anawaambia wananchi kuwa kwa miaka minne imeweka rekodi kwenye kufanikisha kasi ya maendeleo vijijini na mapinduzi makubwa ya kilimo.

Akianza na maendeleo vijijini anasema, moja ya urithi mkubwa wa wananchi vijijini kufanikisha kilimo cha mazao zaidi kuanzia mpunga, chai, kahawa, kakao, maharage na mahindi yanayostawi kutokana na kupewa ruzuku ya pembejeo ya mbolea, mbegu na masoko ya uhakika.

Lakini pia awamu hiyo imefanikisha ujenzi wa barabara za lami vijijini kwenye mashamba ya wakulima na kazi hiyo ikifanyika Rungwe, anataja baadhi ya barabara zenye lami kuwa ni Ndulilo kwenda Utete yenye taa pia. 

Nyingine ni ya kutoka Ruangwa kwenda Kejo ambayo ina taa za barabarani ikiwaunganisha wakulima na miundombinu ya usafiri kwenda maeneo mbalimbali. 

Anasema pamoja na juhudi hizo ameongeza kasi ya maendeleo vijijini kuanzia elimu, afya maji na serikali ya Dk. Samia ameongeza huduma nyingi zikiwamo za afya, nishati, elimu na maji.

Akinukuu takwimu za maendeleo ya afya zinazoonesha kuwa awamu ya tatu ilijenga vituo vya afya 105, ya tano ilijenga 446 na awamu ya sita imeongeza vituo hadi kufikia 1,000.

“Moja ya urithi mkubwa kwa wananchi anaoucha Rais Samia ni maendeleo vijijini. Nilikuwa nasoma insha ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ya Septemba 1967 na hapa namnukuu.”

Tanzania Tunayoitaka ndicho kichwa cha insha yake, anasema kwa miaka mingi ijayo wananchi wengi wataendelea kuishi vijijini na kujipatia ruzuku kupitia kilimo, hii ndiyo kusema lazima kujenga utaratibu wa kuinua maisha yao.

Tunavyozidi kuendelea huduma zinazopatikana mjini lazima ziwafikie wananchi na wakulima vijijini ...” anasema.

Anaongeza kuwa Baba wa Taifa hakuishia hapo alianzisha Wizara ya Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini ili kufanikisha azma hiyo. 

Anawaambia wananchi kuwa Rais Samia ameendelea kusimamia ajenda hiyo na kuhakikisha kuwa maendeleo yanafikishwa vijijini na kufikia azma ya Tanzania Tunayoitaka. 

JOTO ARDHI

Profesa Kabudi anazungumzia mikakati ya kuongeza nishati akisema kuwa Tanzania itaanza kutumia umeme wa joto ardhi linalopatikana ndani ya bonde la ufa linalopita eneo la Rungwe.

Anasema kuwa awamu ya sita imeanza mikakati ya kutekeleza maradi wa kuvuna joto hilo ili kupata nishati jadidifu.

Anaeleza kuwa moja ya kichocheo cha maendeleo duniani ni nishati ya uhakika, salama na bora ambayo itachangia uzalishaji wa bidhaa bora kwa gharama nafuu, kutumiwa nyumbani na kutunza mazingira.

Profesa Kabudi, anasema katika mkutano huo uwekezaji huo, utaanza na kuwanufaisha kwaza wana Rungwe.

Anasema Rungwe ndiyo ya kwanza kutoa umeme wa joto ardhi na watumiaji wa mwanzo wa nishati hiyo watakuwa ni wananchi wa eneo hilo

Anawaeleza kuwa joto ardhi linalopatikana katika bonde la ufa, tafiti zimeonesha kuwa lina nishati jadidifu nyingi ya uhakika, safi, isiyochafua mazingira na endelevu na kwamba Tanzania imejaliwa rasilimali hiyo ambayo serikali itakayochaguliwa itaaendeleza uwekezaji.