Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya, ametoa wito kwa Waziri wa Maji, Juma Aweso, kuhakikisha taasisi zote za umma zinazodaiwa malimbikizo ya ankara za maji zinakatwa huduma, kama inavyofanyika kwa wananchi wa kawaida.
Akizungumza Mei 8, 2025 bungeni jijini Dodoma, wakati wa mjadala wa makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Bulaya amesema taasisi hizo zina deni linalofikia takriban shilingi bilioni 61, hali inayokwamisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wengine.
“Mhe. Naibu Spika, mimi mwenyewe nimewahi kukatiwa huduma ya maji kwa deni dogo tu, siyo jambo jema kuona wananchi wa kawaida wanadaiwa shilingi 10,000 tu na wanakatiwa huduma, ilhali taasisi kubwa zinazodaiwa mabilioni zikiendelea kupata huduma hiyo bila kulipa,” alisema Bulaya.
Amesisitiza kuwa usawa katika utoaji wa huduma ni muhimu, na kwamba taasisi hizo haziwezi kuachwa ziendelee kutumia maji bure huku wananchi wa kipato cha chini wakihangaika kupata huduma hiyo ya msingi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED