Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, ameiagiza idara ya ardhi ya Halmashauri ya Mji wa Babati, mkoani Manyara, kumpatia mwalimu mstaafu, Zacharia Basso, viwanja vyake 15 ili aviendeleze, aviuze au kufanya shughuli zake za maendeleo.
Kaganda alitoa agizo hilo jana wakati akisikiliza kero za wananchi na kuzitatua. Mwalimu Basso alilalamikia kuwa wataalamu wa ardhi walimnyima fidia ya viwanja 15 ambavyo tayari vilikuwa na umiliki halali, huku viwanja nane vikijengwa bila idhini yake, licha ya Mkurugenzi wa Halmashauri kumrejeshea umiliki wa baadhi ya viwanja hivyo.
Awali, mstaafu huyo alimueleza mkuu wa wilaya kuwa alikuwa na viwanja 76 na Halmashauri iliahidi kumpatia fidia ya viwanja 15, lakini hakupati fidia hiyo. Badala yake, alishutumu kwamba aliishia kutishiwa maisha na baadhi ya watu waliokuwa wanamiliki na kujenga kwenye viwanja vyake.
“Nataka mniletee watu waliojenga kwenye viwanja vinne na alipwe fidia ya viwanja vingine 11,” alisema Kaganda, akiagiza hatua za utekelezaji wa kisheria iwapo waliojenga hawatalipia.
Aidha, Kaganda aliagiza mwalimu Basso afike ofisi za ardhi ili kukaa meza moja na walionunua pamoja na wataalamu wa ardhi ili majadiliano ya fidia yaweze kufanyika kwa utaratibu. Alisisitiza kuwa nyaraka zote za umiliki wa viwanja lazima ziwepo siku ya majadiliano.
Mwalimu Zacharia Basso alimshukuru mkuu wa wilaya kwa kusikiliza kero yake na kuchukua hatua za kuhakikisha haki yake inatimizwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED