Kampuni ya Sweden kuwekeza teknolojia ya umwagiliaji nchini

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 02:47 PM Sep 20 2025
Balozi wa Tanzania nchini Sweden,Mobhare Matinyi, akijadiliana na maafisa watendaji wa kampuni ya SPOWDI, Henrik Johanson (katikati) na Christopher Thunell (kulia) katika ofisi za Ubalozi jijini Stockholm, t Septemba 18, 2025.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Balozi wa Tanzania nchini Sweden,Mobhare Matinyi, akijadiliana na maafisa watendaji wa kampuni ya SPOWDI, Henrik Johanson (katikati) na Christopher Thunell (kulia) katika ofisi za Ubalozi jijini Stockholm, t Septemba 18, 2025.

Balozi wa Tanzania katika nchi za Nordic, Baltic na Ukraine, Mobhare Matinyi, alikutana na watendaji wa kampuni ya SPOWDI, Henrik Johanson na Christopher Thunell, katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Stockholm, Sweden, kujadiliana kuhusu uwekezaji wa teknolojia ya kilimo makini cha umwagiliaji nchini.

Teknolojia hiyo ya kampuni ya SPOWDI hutumia mashine ndogo ya nishati ya jua yenye mipira ya umwagiliaji inayosambazwa shambani kutokea kwenye bwawa dogo. Umwagiliaji huo hufanyika kwa dakika 15 katika eneo la mita za mraba 500 kwa mara moja.

“Ekari moja yenye mita za mraba 4,000 inaweza kumwagilia kwa muda mfupi tu na kuokoa upotezu wa maji, muda na pia kusaidia mimea kukua kwa ubora unaostahili na hatimaye kutoa mazao mengi zaidi,” amesema Ofisa Mtendaji Mkuu Johanson na kuongeza kuwa matokeo yake ni kuongeza kipato na pia kulima kwa zaidi ya msimu mmoja kwa mwaka kwa gharama nafuu na bila kutegemea mvua.

Kampuni hii inakusudia kuwekeza nchini Tanzania baada ya kuvutiwa na mazingira mazuri ya Tanzania, uchapakazi wa Watanzania na sera nzuri za serikali katika uendelezaji wa sekta ya kilimo ikiwemo kusaidia upatikanaji rahisi wa mikopo kwa wakulima.

Tayari kampuni hiyo imeifikisha teknolojia hiyo katika nchi za Sweden, India, Nepal, Bangladesh, Uswizi na kwa Afrika imeanza uwekezaji nchini Kenya na hivyo Tanzania itakuwa nchi ya pili.

Matinyi aliikaribisha kampuni hiyo kufanya ziara Tanzania mwezi Novemba 2025 ili kuitambulisha teknolojia hiyo na kuanza majaribio ya awali akielezea kwamba hii itakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya serikali ya kuongeza pato la taifa, kupambana na umaskini, kuongeza ajira na uzalishaji na kuuza chakula nje ya nchi baada ya nchi kufikia usalama wa chakula kwa asilimia 140.