Kahyarara: Tanzania imeona fursa kuinua uchumi kwa usafiri wa anga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:48 AM Sep 20 2025
news
Picha Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof.Godius Kahyarara

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof.Godius Kahyarara amesema uchumi mkubwa wa Nigeria umeivutia Tanzania kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Lagos.

Akizungumza leo Septemba 19,2025 wakati wa uzinduzi wa safari ya Dar es Salaam kwenda Lagos,Nigeria, ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), amesema wameona fursa kubwa ya kufungua uchumi na biashara baina ya nchi hizo.

Amesema Tanzania imeona matokeo makubwa baada ya kufungua biashara ya Afrika Kusini kupitia usafiri wa anga, na sasa inaangazia masoko mengine.

"Kwanini Lagos ni kwasababu ya uchumi mkubwa wa Nigeria,ni nchi ya pili kwa uchumi mkubwa Afrika, lakini kuna vipimo vingine Nigeria inakuwa iko juu ya Afrika Kusini kiuchumi,"amefafanua.

"Lakini tumeona matokeo makubwa ya kwenda Afrika Kusini,kwa hivi sasa Tanzania inafanya biashara sana na Afrika Kusini kuliko nchi za Afrika Mashariki,tunaimani kuna fursa kubwa kufungua uchumi na biashara,"amesema.

Prof.Kahyarara amesema pia kuna fursa za wawekezaji wakubwa na ukuaji wa sekta ya utalii ambapo Afrika Kusini na Nigeria zinashindana kwa kuwa na watalii wengi.

"Afrika Kusini tumetumia fursa,,tukiongeza na Nigeria itaongeza sana soko la watalii hasa ndani ya Bara la Afrika na itaongeza uimara kuliko kutengemea masoko ya mbali.Huu ni mkakati wa kiuchumi,"amesema.

Prof.Kahyarara amesema sekta ya anga Tanzania imeendelea kukua na kufanya vizuri na kwamba kwa mwaka huu wa fedha imetengwa bajeti ya kununua ndege kubwa nyingine.

Aidha,amesema katika kuimarisha usafiri wa anga wamefufua nyingine nne za Air Bus ilizokuwa zimeegeswa kwa muda mrefu.

"Tumejipanga baada ya Lagos ni Accra alafu Abijan,tumejipanga vyema kudaka fursa zote Afrika Magharibi na kwingine,"amesema.