Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha UDP, Saum Rashid, amesema endapo wananchi watakiamini chama chake na kukipa ridhaa ya kuunda serikali, watatenga fedha kujenga soko kubwa la kimataifa la mafuta ya alizeti katika Mkoa wa Singida, ili wakulima wapate soko la uhakika la zao hilo.
Akizungumza leo, Septemba 19, 2025, na wananchi katika soko la Misufini, Singida Mjini, Saum amesema Mkoa wa Singida ni maarufu kwa uzalishaji wa alizeti, lakini changamoto kubwa imekuwa ni wakulima kushindwa kupata soko la uhakika kwa mazao yao.
Amebainisha kuwa UDP imejipanga kukuza sekta ya kilimo, ikizingatiwa kuwa kilimo kinashirikisha wananchi wengi, na kitaleta tija kubwa kwa wakulima na taifa kwa ujumla.
“Tutaanzisha mashamba darasa ya kilimo cha alizeti ili kuhakikisha zao hili linazalishwa kwa ubora zaidi na liweze kutosheleza viwanda vya kusindika mafuta ya alizeti vitakavyojengwa. Hatutaki mkulima abaki na mazao shambani bila soko,” amesema Saum.
Mgombea huyo ameongeza kuwa serikali ya UDP itahakikisha uwekezaji mkubwa unaelekezwa katika zao la alizeti kwa lengo la kuongeza thamani na kufungua fursa za ajira na biashara kupitia mnyororo wake wa thamani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED