WAKATI Mgombea urais wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan akitarajia kutua kesho mkoani Ruvuma kuendelea na kampeni za Uchaguzi Mkuu, maandalizi ya kumpokea yameiva.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, amethibitisha hilo leo Septemba 20, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua maandalizi hayo katika uwanja wa Veta akiwa ameambatana na Mgombea Mwenza, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa ajili ya kumpokea mgombea huyo.
Kwa mujibu wa Oddo, Dk. Samia anatarajiwa kuwasili kesho Septemba 21 katika Uwanja wa Ndege wa Songea, ambako atapokelewa na Mgombea Mwenza Balozi Dk. Nchimbi, viongozi wa chama pamoja na wananchi wa mkoa huo.
Amesema ziara yake itaanzia wilayani Nyasa, ikiwemo kusimama Mbinga kuzungumza na wananchi na kisha kufanya mkutano mkubwa wa kampeni katika eneo la Mbamba Bay.
Amesema, Septemba 22 Dk. Samia atafanya mkutano mjini Songea katika viwanja vya Veta ilivyopo Msamara, kabla ya kuelekea Namtumbo na Tunduru.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED